Nov 27, 2023 02:43 UTC
  • Jumatatu tarehe 27 Novemba 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Jamadil Awwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Novemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Bibi Fatimatu Zahra binti wa Mtume Muhammad (saw) alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa mafunzo makubwa ya kimaadili na kimaanawi. Baba yake ni Mtume Muhammad (saw) na mama yake ni Bibi Khadija Binti Khuwaylid (as). Bibi Fatima alishiriki katika medani mbalimbali za mapambano mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu akiwa bega kwa bega na baba yake, Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Talib pamoja na watoto wake wema, yaani Imam Hassan na Hussein (as) ambao Mtume amewataja kuwa ni vinara wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatima alisifika kwa tabia njema, uchamungu, elimu na maarifa, na alikuwa mfano na kigezo chema cha mwanamke na Waislamu kwa ujumla.   

Katika siku kama ya leo miaka 1373 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ibrahim bin Malik al Ashtar mmoja wa makamanda na mashujaa wa Uislamu aliuawa katika vita na jeshi la Bani Umayyah. Alikuwa mtoto wa Malik al Ashtar, Swahaba na kamanda wa jeshi la Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as). Ibrahim alikuwa pamoja na baba yake katika kipindi cha ujana katika vita vya Siffin na alionesha ushujaa mkubwa dhidi ya jeshi la Muawiyyah.  Ibrahim Malik Ashtari aling'ara zaidi katika harakati iliyoanzishwa na Mukhtar Thaqafi huko Kufah dhidi ya utawala dhalimu wa bani Umayyah. Harakati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kulipiza kizazi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) pamoja na masahaba zake waliouawa katika tukio la Karbala mwaka 61 Hijria.  

Tarehe 27 Novemba miaka 104 iliyopita iliainishwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya kumalizika vita hivyo na kutiwa saini mkataba wa amani wa Versailles kulisainiwa mikataba mingine kadhaa ya kuainisha mustakabali wa tawala za Austria na Hungary na utawala wa Othmania na nchi ya Bulgaria ambayo kila mmoja ulikuwa na masharti mazito na kutoa fidia nchi hizo kwa zile zilizopata ushindi. Kuainishwa kwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati katika mkutano wa Paris kulibadili kikamilifu ramani ya dunia.   

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo. Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti.   

Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchill na Joseph Stalin 

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Eugene O’Neill mwandishi Kimarekani. Eugene O’Neill ambaye alikuwa mashuhuri pia katika uandishi wa tamthilia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65. Alizaliwa mwaka 1888 na maisha yake yalitawaliwa na matukio mengi. Eugene O’Neill alikuwa na mapenzi makubwa na tamthilia na ndio maana akapewa jina la mtoto wa tamthilia. Mwaka 1936 Eugene O'Neill alitunukiwa tuzo ya Nobel. Baadhi ya vitabu vya mwandishi huyu ni Mfalme Jones, The First Man na Days Without Ends.   

Eugene O’Neill