Nov 28, 2023 23:24 UTC
  • Jumatano, Novemba 29, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1445 Hijria sawa na Novemba 29 mwaka 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1407 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. 

Tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria, yaani miaka 1407 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka. 

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo. Gazeti hilo lilisimamishwa mwezi Dhilhija mwaka huo huo baada ya kuchapishwa kwa kipindi cha miezi kadhaa tu katika nchi za Ulaya, India, Misri, Iran na katika nchi kadhaa za Kiarabu kutokana na mashinikizo ya kisiasa ya baadhi ya nchi.

Sayyid Jamaluddin Asadabadi

Miaka 80 iliyopita sawa na tarehe 29 Novemba 1943 harakati ya Ukombozi ya kupambana na ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Marshal Tito. Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani. Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya kupambana na ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.  

Marshal Tito

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita mwafaka na tarehe 29 Novemba 1947, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi hafifu wa kura suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi. Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.   

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 8 Azar mwaka 1373 alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na tangu akiwa na umri mdogo alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza elimu ya dini. Ayatullah Muhammad Ali Araki kwa muda mrefu alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum na miongoni mwa vitabu vyake ni risala ya Ijitihadi na Taqlidi pamoja na Sherhe ya Uruwatul Uthqaa.   

Ayatullah Muhammad Ali Araki

Na miaka 13 iliopita sawa na tarehe 8 mwezi Azar mwaka 1389 Hijria Shamsia, Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi waliokuwa Wahadhiri wa Fizikia ya Nyuklia wa Iran walilengwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi mjini Tehran. Dakta Abbasi alijeruhiwa ambapo Dakta Majid Shahriyari Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Mwanafizikia na Msomi wa Nyuklia wa Iran akauawa shahidi katika shambulio hilo. Magaidi waliofanya jinai hiyo walitiwa nguvuni na kukiri kwamba wanashirikiana na shirika la ujasusi la Israel MOSSAD.

Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi