Alkhamisi, Novemba 30, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria, mwafaka na tarehe 30 Novemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 1164 iliyopita alifariki dunia Abu Hanifa Dinawari, mtaalamu wa fasihi, nujumu na mwanahisabati wa Kiislamu. Abu Hanifa Dinawari ni mmoja wa wanafalsafa na wataalamu wa theolojia na wanahisabati wa zamani wa ulimwengu wa Kiislamu ambaye alizaliwa mjini Kermanshah yapata mwaka 222 Hijiria. Alikuwa msomi mashuhuri katika kipindi cha utawala wa Samanid huku akitabahari katika elimu za nahw, lugha, mantiki, nyota, elimu ya maumbo, uhandisi na kadhalika. Mbali na hayo pia Abu Hanifa Dinawari alikuwa mtaalamu wa elimu ya mimea, historia, jografia, nyota, hisabati na kadhalika. Moja ya athari maarufu za mwanazuoni huyo ni pamoja na 'Kitaabun-Nabaat' ambacho kimejikita katika kutambua mimea, 'Al-Akhbaaru al-Twiwaal' 'Al-Faswaahah' 'Al-Shiiru wa Al-Shuaraa' na 'Al-Buldaan.'

Miaka 356 iliyopita katika siku kama ya leo, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78.
Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitababu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ndiyo kitabu kamili cha historia ya mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 na alifariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86.
Miaka 188 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Mark Twain mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Twain alikipitisha kipindi cha utoto na ubarobaro wake na matukio yasiyo ya kawaida ambayo baadaye yalikuja kuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain alikuwa mwandishi mwenye utani na mzaha. Aliandika visa na simulizi nyingi kwa ajili ya watoto na vijana wadogo ambapo tunaweza kuashiria hapa vitabu vyake viwili vya The Andventures of Tom Sawyer na (Matukio Yasiyo ya Kawaida ya Tom Sawyer) The Prince and The Pauper (Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Ombaomba). Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na ukata na umasikini mkubwa na hatimaye akaaga dunia mwaka 1910 baada ya kuugua.
Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Oscar Wilde, mwandishi na malenga mahiri wa Ireland. Wilde alizaliwa mwaka 1854 katika familia iliyokuwa na mapenzi maalumu na masuala ya kiutamaduni na Sanaa. Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu. Oscar Wilde alianza kujihusisha na taaluma ya uandishi akiwa katika rika la ujana na katika kipindi kifupi cha umri wake alifanikiwa kuandika vitabu mbalimbali vilivyokuwa na madhumuni ya riwaya, mashairi na maigizo. Baadhi ya vitabu vya Oscar Wilde ni The Model Millionaire, The Soul of Man Under Socialism na The Canterville Ghost.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad katika mji wa Cairo nchini Misri. Abdul Basit alikuwa mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Alianza kujifunza Qurani Tukufu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Katika maisha yake Ustadh Abdul-Basit alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya qiraa ya Qur'ani Tukufu.
Siku ya leo inayosadifiana na tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya huadhimiwa hapa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Sheikh Mufid, alimu, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kishia. Alimu huyu ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Mufid, jina lake kamili ni Muhammad bin Nu'man na alizaliwa huko Baghdad mwaka 336 Hijria. Alionyesha kipaji kikubwa cha masomo na ufahamu tangu akiwa katika rika la utoto na ni katika kipindi hicho pia alipoanza kusoma masomo ya Kiislamu. Sheikh Mufid ameandika vitabu vingi ambavyo vinakadiriwa kufikia 200. Al'Alam, Amali na Irshad ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya Sheikh Mufid. Alimu huyu amezikwa huko Kadhimain nchini Iraq.
