Dec 01, 2023 10:07 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (38)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 38 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 38.

أَشْرَفُ الْغِنَى، تَرْکُ الْمُنَى

Utajiri bora kabisa ni kudhibiti matamanio.

Wasikilizaji wapenzi, katika hikma hii ya 38 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatoa maelelezo mafupi lakini yenye maana pana. Anatoa somo kubwa kwa kila anayesaka utajiri wa kweli na kukinai. Anasema, mtafutaji wa utajiri wa kweli na kutokuwa na haja na viumbe bali kumtegemea kikwelikweli Muumba, ni yule anayefanikiwa kuachama matamanio na hawa za nafsi yake. 

Rajwa na matumaini yenyewe kama yenyewe ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya viumbe wake. Kimsingi, mwanadamu anaishi na matumaini. Usiku, anapokwenda kulala analala kwa matumaini na huwa anatamani siku inayofuata itakuwa imejaa furaha na mafanikio, na anaamka asubuhi akiwa na matumaini ya jua kuchomoza tena na siku iliyojaa furaha. Mwanadamu hawezi kutenganishwa na matumaini, rajwa na matarajio kwa sababu ameumbwa kwa namna ambayo matamanio hayo yako pamoja naye na yamewekwa kwa kawaida na kwa kawaida na kwa haki katika kuwepo kwake. Mwanadamu amepewa uwezo wa kuhisi ladha, macho, masikio, na hisia za kutambua vitu mbalimbali. Lazima mwanadamu atatafuta kuridhisha hisia zake za kuonja, kuona, kusikiliza hisia nyiunginezo. Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu na nguvu mwilini ambazo zinamlazimisha aoe au aolewe. Amemuumba mwanadamu kwa namna ambayo lazima mume na mke waishi pamoja kwa ajili ya kuendeleza kizazi cha mwanadamu, na amejaalia mapenzi maalumu baina ya mume na mke. Ndani ya mapenzi hayo mnapatikana kizazi cha watoto lakini yote hayo mwanadamu anayafanya kwa matumaini. Hakuna yeyote mwenye yakini kwamba atapata mke wa kuoa au mume wa kuolewa naye, lakini matumaini hayo hayaachi. Kila mwanadamu ana matumaini kwamba katika ndoa atapata watoto, lakini hayo ni matumaini tu si yakini, kwani hakuna yeyote mwenye yakini kwamba katika ndoa yake hiyo atapata watoto. Kila mwanadamu anajitahidi sana kulea watoto wake kwa matumaini kwamba watamsaidia uzeeni na watakuwa watu bora katika jamii, lakini hayo pia ni rajwa na matumaini, si yakini. Hivyo ni muhali kwa mwanadamu kutenganishwa na matumaini. 

Baada ya kuukiri ukweli huo tunapenda kusema kwamba, anachopaswa kuzingatia mwanadamu ni kuhakikkisha kwamba matumaini na tamaa zake hazichupi mipaka. Hamu na matumaini ni mambo ambayo yanapaswa kuendana na juhudi za mtu. Kwa mfano mtu anapolima shamba na kutengeneza bustani, hufanya hivyo kwa matumaini ya kuwa na  bustani ya kijani kibichi na yenye matunda ya kufurahisha. Lakini matumaini hayo hayafanikiwi kama hatofanya juhudi na jitihada kubwa katika ukulima wake na kufanya kazi kwa utaalamu na kufuata njia sahihi zinazotakiwa. 

Lakini wakati mwingine matumaini na tamaa haziwiani na kiwango cha uwezo na kipaji tulichopewa wanadamu na hayaendani na kipindi kifupi cha maisha yetu. Uislamu umetukataza kuwa na tamaa zinazochupa mipaka. Kwa sababu tamaa za kuchupa mipaka haziiingii akilini kabisa, si za kimantiki na ni muhali kufikiwa. Bila shaka tamaa ya kuchupa mipaka inampokonya mwanadamu nguvu za kuamua na kuwa huru kwa sababu kwa upande mmoja anakuwa na tamaa ya kufikia jambo ambalo ni muhali kufikiwa na kwa upande mwingine humkosesha mtu uhuru wa kufikiri vizuri na kuwa na maamuzi ya kimantiki kutokana na kugubikwa tu na tamaa ya kupindukia na kujidanganya kuwa atafikia matamanio yake hayo. Mara nyingi hutokezea pia mtu mwenye tamaa kupindukia anafuja rasilimali zake nyingi kwa tamaa ya kupata kitu kikubwa zaidi lakini matokeo yake huwa ni kuangamia na huwa ni sawa na ule usemi wa tamaa mbele, mauti nyuma. Na ndio maana Imam Ali AS akatuusia katika hikma hii ya 38 ya Nahjul Balagha akisema: Utajiri bora kabisa ni kudhibiti matamanio.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags