Jumatatu 4 Disemba, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Jamadil Awwal 1445 Hijria sawa tarehe 4 Disemba 2023.
Tarehe 20 Jumadil Awwal mwaka 682 katika siku kama ya leo miaka 763 iliyopita, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa katika mji wa Hilla nchini Iraq na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama hizo. Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali kama fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, usulul fiqhi na teolojia. Miongoni mwa vitabu vya mwanazuoni huyo ni Al Kafiyah na Tahswilul Najah.

Miaka 124 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina.

Miaka 12 iliyopita katika siku hii, tarehe 13 Azar 1390 Hijiria Shamsiya: Mamlaka ya kijeshi ya Iran ilitangaza kuidhibiti ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani au drone aina ya RQ-170 mashariki mwa Iran. Ndege hii iliyokuwa imepaa kutoka kambi yake nchini Afghanistan, iliangukia kwenye mtego wa vitengo vya vita vya kielektroniki vya Iran katika kina cha kilomita 200 ndani ya Iran na iliangushwa ikiwa na uharibifu mdogo. Ndege hiyo ya RQ-170 ni mojawapo ya ndege za kisasa zaidi zisizo na rubani za Jeshi la Marekani.
Kwa hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuchukua udhibiti wa ndege ambayo ina uwezo wa kukwepa rada ilionyesha uwezo wake katika uwanja wa vita vya kielektroniki na kusababisha mshangao mkubwa miongoni mwa wataalamu wa kijeshi na mkanganyiko katika safu za watawala wa Marekani. Baada ya miaka mitatu, wataalamu wa Iran waliweza kunakili teknolojia ya uundaji wake na miaka mitatu baadaye walitengeneza mfano wake kamili.