Dec 08, 2023 22:54 UTC
  • Jumamosi, 09 Disemba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 9 Disemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 281 iliyopita Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo. Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni. Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine. ***

Carl Wilhelm Scheele

 

Miaka 265 iliyopita vilianza vita vya miezi 13 vya Madras. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India. Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22. Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita yaani tarehe 9 Disemba mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru. Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipopata uhuru na kujitawala katika siku kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika. Mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ***

 

Siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu. Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao. ***

Intifadha

 

Miaka 32 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980. Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi.