Dec 22, 2023 02:29 UTC
  • Leo ni Ijumaa, tarehe 22 Disemba, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Mfunguo Tisa Jumadithani 1445 Hijria sawa na tarehe 23 Disemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 2,169 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge.

Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania. 

Miaka 384 iliyopita  katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa.

Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699 Miladia. 

Jean Racine

Katika siku kama ya leo miaka 330 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia.

Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo.

Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.   

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin A'mili, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu.

Ayatullah Sharafuddin alizaliwa mwaka 1290 Hijria huko Kadhimain moja kati ya miji ya Iraq. Alielekea Jabal A'mil nchini Lebanon baada ya kuhitimu masomo yake na kuanza kujishughulisha na harakati za Kiislamu.

Msomi huyo mkubwa ametoa huduma za thamani kubwa kwa Ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa akisisitiza suala la umoja baina ya Waislamu. Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin ameandika vitabu na risala nyingi ili kufikiwa lengo hilo.

Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin A'mili

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo.

Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Mfereji wa Suez.

Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Mfereji wa Suez, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri ya kutangaza kutaifisha mfereji huo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo, na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.   

Bandari ya Port Said mwaka 1880

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989 Miladia, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa.

Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.   

Nicolae Ceausescu