Dec 24, 2023 02:33 UTC
  • Jumapili, 24 Disemba, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 10 Mfunguo Tisa Jamadithani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 24 Disemba 2023 Miladia.

Miaka 818 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe 10 Jumadithani kwa mujibu wa nukuu za kuaminika za historia alifariki dunia arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Sheikh Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa mwaka 513 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Baadhi ya nukuu za kihistoria zinasema msomi huyo kubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi katika mashambulizi ya Mogul. Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiq al-Twair."***

 

Miaka 499 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498 baharia huyo mashuhuri wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India. ***

Vasco da Gama

 

Miaka 174 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya Ufaransa yaliishambulia ardhi ya Guinea ya magharibi mwa Afrika. Mashambulio hayo yalikuwa utangulizi wa Ufaransa kudhibiti ardhi hiyo iliyokuwa na utajiri wa dhahabu. Kabla ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia ardhi ya Guinea, kulikuwa kumeanzishwa mashirika ya kibiasharaya dhahabu katika pwani ya Guinea. ***

Bendera ya Guinea

 

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi. Hata kama kundi la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limeshafanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao. ***

Ku-Klux-Klan

 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi kuteuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Miladia Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951. ***

Bendera ya Libya

 

Tags