Dec 28, 2023 23:00 UTC
  • Ijumaa, tarehe 29 Disemba, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Jumadithani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Disemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1409 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilitokea vita vya Jamal baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina.

Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu.

Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair wakiandamana na Bibi Aisha binti Abu Bakr, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 674 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu.

Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.   

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa ilitiwa saini na kupasishwa na mfalme wa wakati huo wa Iran Mozaffar ad-Din Shah Qajar.

Katiba hiyo ilikuwa na vipengee 51 ambapo baadaye viliongezwa vipengee 107 kama vikamilisho.

Katika kipindi cha miaka iliyofuata na katika zama za tawala mbalimbali hususan katika kipindi cha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho ya kimsingi. Akthari ya marekebisho hayo yalikuwa ni9 kwa madhara ya mamlaka ya wananchi na Uislamu.

Miaka 93 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Theodor Nöldeke msomi wa Kijerumani na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki.

Alihitimu masomo yake katika taaluma ya teolojia, falsafa pamoja na lugha mbalimbali na kutunukiwa shahada ya uzamivu. Theodor Nöldeke alianza kufundisha Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 na kuifanya kazi hiyo kwa miaka mingi.

Theodor Nöldeke alikuwa amebobea katika lugha za Kiarabu, KIifarsi, Kituruuki, Kigiriki, Kihispania na Kitaliano. 

Theodor Nöldeke

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza.

Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza.

Uhuru wa Ireland ulikuwa matokeo ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.