Dec 30, 2023 02:30 UTC
  • Jumamosi, 30 Disemba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Tisa Jamadithani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 30 Disemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1024 iliyopita, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mwashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania. ***

Ibn Darraj Qastalli

 

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo. ***

Miaka 45 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo. ***

 

Shapour Bakhtiar

 

Tarehe 30 Disemba miaka 17 iliyopita Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraq, alinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi ikiwemo Marekani.  ***

Saddam

 

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba, yaani miaka 14 iliyopita, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. wa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali". ***

Tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali