Dec 30, 2023 22:56 UTC
  • Jumapili, 31 Disemba, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Tisa Jamadithani 1445 Hijria sawa na tarehe 31 Disemba 2023 Miladia.

 

Miaka 858 iliyopita katika siku kama ya leo kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre (Akka) katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo. Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 497.  Mwaka 583 mji huo ukakombolewa na Salahuddin Ayubi.***

Salahuddin Ayubi

 

Tarehe 31 Disemba mwaka 1994 yaani miaka 29 iliyopita, Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliasisiwa kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika. Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service. ***

Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussain Nuri. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi na mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu. Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Beiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman". Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. ***

Hajj Mirza Hussain Nuri

 

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita iliundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kote duniani, kujenga uhusiano baina yao, kunyanyua juu kiwango cha shule za kidini, kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza baina ya wafusi wa Ahlul Bait na madhehebu nyingine za Kiislamu na kadhalika. ***

Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait

 

Katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia. ***

Rais Boris Yeltsin wa Russia