Jan 04, 2024 02:35 UTC
  • Alkhamisi, Januari 4, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Mfunguoi Tisa, Jamadithani 1445 Hijria sawa na 4 Januari mwaka 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1061 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Jamaduth-Thani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi ya mashairi. Aidha kwa muda mfupi Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kisha akajishughulisha na kazi ya ukadhi. Kitabu cha ‘al Faraj Baada sh-Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Kitabu kingine cha msomi huyo ni ‘Al-Masaajid’ ambacho hekaya na masuala ya akhlaqi na maadili mema.

Siku kama ya leo miaka 451 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa

*Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka ya kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo.

Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyoendelea kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya.   

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika.

Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika.  

Casablanca. Morocco

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za Marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa.

Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran, Shah Pahlavi, ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekuwa na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi.

Hata hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran na uliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.

Mkutano wa Guadeloupe

Tarehe 14 Dei miaka 45 iliyopita wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasiri kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.

Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran. 

Jenerali Robert E. Huyser

Tarehe 4 Januari miaka 13 iliyopita alifariki dunia Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga wa Tunisia, siku 18 baada ya kujichoma kwa moto katika mji wa Buzid akilalamikia ukandamizaji na dhulma ya serikali ya nchi hiyo.

Kujichoma moto kijana huyo muuza mboga kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa nchi hiyo na kuwa sababu ya kupinduliwa dikteta Zainul Abidin bin Ali.

Kitendo hicho cha Bouazizi pia kilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.

Mohamed Bouazizi