Jan 04, 2024 07:41 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (39)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 39 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ijapokuwa hii ni sehemu ya 39 ya mfululizo huu, lakini hii ni Hikma ya 35.

مَنْ أَسْرَعَ إِلَى النَّاسِ بِمَا یَکْرَهُونَ، قَالُوا فِیهِ [مَا] بِمَا لَا یَعْلَمُون

Anayekimbilia kufanya mambo yanayowachukiza watu, watamsema kwa ambayo hawayajui.

Naam, wasikilizaji wapenzi, katika hikma hii ya 35 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anawausia watu kuchunga sana maneno na matendo yao akisema, mtu anayeharakisha kufanya jambo ambalo watu hawalipendi, ikawa kwa mfano anazungumza bila ya kufikiri au kufanya kitu kinyume na mapenzi na matakwa yao atambue kuwa watu hao watamsema kwa mambo ambayo na yeye hayafurahii. Sababu yake ni kuwa, unapomuumiza mtu, huwa umejiondolea kinga kwa yeye kujali anachokisema juu yako na jiandae kusikia na kuona chochote kutoka kwake. 

Imam Ali AS anasema katika Hikma hii ya 35 ya Nahjul Balagha kwamba: Anayekimbilia kufanya mambo yanayowachukiza watu, watamsema kwa ambayo hawayajui.

 

Moja ya masuala muhimu sana ya kuzingatiwa katika mlahaka na muamala na watu ni jinsi wanavyoamiliana wao kwa wao. Ni mlahaka na maingiliano ya mtu na wengine. Tatizo linakuja pale matukufu na thamani za mtu muumini zinapokuwa haziwiani na matakwa, mila na desturi za watu waliomzunguka. Kwa maneno mengine, kuna wajibu wa kuwa mwangalifu na kutofanya kitendo bila kujali, au kutenda mambo kinyume na imani na mtazamo wa wengine, kwani kufanya hivyo hujenga mazingira ya kutolewa hukumu isiyofaa dhidi ya mtu wa aina hiyo. Kuna udharura wa kuzingatia mila na desturi za watu, kuheshimu sheria za kiraia, mila na desturi zilizokita mizizi za jamii fulani ya watu, imani na itikadi jumla, utamaduni unaotawala jamii, vyote hivyo vinamwajibisha mtu mwenye hikma kuwa mwangalifu sana katika maneno na matendo yake akitambua kwamba, kosa dogo tu, linaweza kusahaulisha mema yake yote na kumfanya aonekane mbaya.

Nukta moja muhimu katika mawasiliano na mwingiliano wa kijamii ni kwamba mtu achukue tahadhari sana wakati anapokumbana na mambo ambayo hata kama yana maslahi kwa watu hao, lakini hayaendani na asili, utamaduni na desturi zao. Mtu anapaswa kwenda polepole na kuwaelimisha kwa busara watu hao kuhusu madhara ya mila na desturi zao na kutoa muda wa kutokea mabadiliko polepole. Kwa hakika Muislamu anatakiwa kuwa mwerevu na azingatie hisia za watu na azungumze kwa namna ambayo hatajeruhi hisia zao. Tab'an hii haina maana kwamba tuache kusema haki na tuzungumze wanavyotaka watu, bali tunapaswa kuwa na busara na kuandaa mazingira mazuri ya kuisema haki na kuifanya ikubalike katika jamii. Suala hilo ni muhimu sana kiasi kwamba kwa mujibu wa aya za 43 na 44 ya Surat Taha, Mwenyezi Mungu anawaamrisha Mitume wake wawili, Nabii Musa na Nabir Harun AS akiwaambia: Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa. Bila ya shaka ni kwa kutegemea mafundisho hayo ya Qur'ani Tukufu ndio maana hapa Imam Ali AS naye anatuusia katika hikma hii 35 kwamba tufanye busara katika maneno, matendo na mlahaka wetu na wengine kwani manufaa yake yanatufikia sisi kwanza hata kabla ya watu wengine. 

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.