Jan 07, 2024 00:59 UTC
  • Jumapili, 07 Januari, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 24 Jamadithani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 7 Januari 2024 Miladia.

Miaka 901 iliyopita, siku ya 24 ya Jumadi al-Thani mwaka wa 544 Hijiria:  "Ahmed bin Ali Beyhaqi Sabzevari" mmoja kati ya wanazuoni wa sayansi ya Qur'ani aliaga dunia  katika mji wa Neyshabur. Alihesabiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake katika elimu ya sarufi na msamiati, na pia alizifasiri na kuzisoma vyema aya za Qur'ani Tukufu. Anakumbukwa kwa maandishi mengi, ikiwa ni pamoja na "Taj al-Masadir kuhusu misamiati na al-muhait bi'ilm al Qur'an". Aghalabu ya vitabu vyake vilikuwa ni kuhusu  Qur'ani Tukufu. ***

"Ahmed bin Ali Beyhaqi Sabzevari"

 

Katika siku kama ya leo miaka 829 iliyopiita aliaga dunia Yahya bin Qassim Tha'labi malenga na mshairi mashuhuri wa Kiarabu ambaye ni mashuhuri kwa lakkabu ya Abu Zakaria. Mbali na kubobea katika elimu fasihi alikuwa mahirii pia katika eliimu za fikihi, lugha na tafsiri ya Qur'an na alihesabiwa kuwa mwanazuoni stadi katika zama zake. Kwa miaka mingi Abu Zakria likkuwa akifundisha katika shule ya Nidhamiiya mjini Baghdad. ***

Yahya bin Qassim Tha'labi malenga na mshairi mashuhuri wa Kiarabu

 

Miaka 88 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wanawake wa Kiirani walipigwa marufuku kuvaa vazi la Kiislamu la aina yoyote kufuatia amri ya Rezakhan Pahlavi. Rezakhan alitoa amri hiyo baada ya kutekelezwa mpango wa kubadili mavazi ya wanaume nchini Iran. Mpango huo ulitekelezwa kwa lengo la kufuta thamani za Kiislamu na badala yake kuiga utamaduni wa Kimagharibi. Ridhakhan alitekeleza mpango huo wa kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu nchini Iran baada ya safari yake nchini Uturuki na kufuata nyayo za Kemal Atatürk Rais wa wakati huo wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi ambaye aliwapiga marufuku wanawake wa nchi hiyo kuvaa mavazi ya Kiislamu. ****

Rezakhan Pahlavi

 

Miaka 81 iliyopita yaani mnamo tarehe 7 mwezi Januari mwaka 1943 aliaga dunia Nikola Tesla mwanafikia mzaliwa waYugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux). ***

Nikola Tesla

 

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Gholamreza Takhti mchezaji na bingwa wa mchezo wa mieleka wa Kiirani aliuawa kwa njama zilizopangwa na utawala wa wakati huo wa Shah. Takhti Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa na maisha ya kati na kati. Gholamreza Takhti alijulikana mno kwa tabia yake ya huruma, ukweli na mapenzi yake kwa watu.  Katika kipindi cha uhai wake na wakati wa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, Gholamreza Takhti alifanikiwa kuipatia Iran medali 9 za dhahabu na fedha katika mashindano ya Olimpiki. Takhti ni miongoni mwa wachezaji wa Kiirani waliotwaa medali nyingi za dhahabu na fedha katika mashindano muhimu ya kimataifa. ***

 Gholamreza Takhti

 

Miaka 46 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran. ***

 

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, majeshi ya Vietnam yaliishambulia Cambodia na kupelekea dikteta wa nchi hiyo Pol Pot kuikimbia nchi hiyo na hatamu za uongozi kuchukuliwa na Heng Samrin. Pol Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge la Cambodia lililokuwa likifuata fikra za Kimao. Katika kipindi cha chini ya miaka mitatu cha uongozi wake nchini Cambodia, Pol Pot akishirikiana na kundi la Khmer Rouge aliwauwa watu kati ya milioni 1.5 na milioni 2.  ***

Pol Pot

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Suleiman Khater mmoja wa polisi wa mpakani katika jangwa la Sinai, alikufa shahidi akiwa jela. Akionyesha upinzani wake dhidi ya mkataba wa Camp David, Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni kadhaa katika jangwa la Sinai. Serikali ya Misri baada ya kumtia mbaroni askari huyo, ilimhukumu kifungo cha maisha jela. Hata hivyo baada ya muda kiwiliwili cha Suleiman Khater kilipatikana katika kituo cha matibabu cha magereza kikiwa kimening'inia na serikali ya Misri ilidai kwamba, mfungwa huyo alijiuwa. ***

Suleiman Khater