Jan 10, 2024 01:11 UTC
  • Jumatano, tarehe 10 Januari, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 27 Jamadithani 1445 Hijria sawa na Januari 10 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya mbalimbali aliaga dunia Hussein bin Ahmad Hajjaj mshairi na malenga mashuhuri wa Kishia. Hussein bin Ahmad Hajjaj aliyekuwa malenga mahiri na mwanafsihi mbobezi, aliishi zama moja na Sayyid Murtadha na Sayyid Radhi wanazuoni na wanachuoni wakubwa wa karne ya nne Hijria. Alikuwa mshairi kipenzi wa Ahlul-Baiti (as) na adui mkubwa wa maadui wa dini na ametunga beti nyingi za mashairi katika uwanja huo.  Hussein bin Ahmad Hajjaj aliaga dunia katika eneo lililopo baina ya Baghdad na Kufa na kwa mujibu wa wasia wake, Ibn  Hajja alizikwa upande wa chini wa miguu Imam Mussa al-Kadhim (as) katika mji wa Kadhmein Iraq.

Katika siku kama ya leo miaka 200 iliyopita inayosadifiana na 10 Januari 1824, Joseph Aspdin mwanakemia wa Uingereza alifanikiwa kutengeneza saruji na kwa utaratibu huo kulipatikana mabadiliko makubwa katika shughuli za ujenzi. 

Hatua hiyo ilitambuliwa kama tukio kubwa katika shughuli za kimaendeleo na ujenzi mpya wa nyumba. Joseph Aspdin ambaye alikuwa akifanya utafiti kwa miaka kadhaa ili kutengeneza mada ambayo ingesaidia kuimarisha msingi wa nyumba, hatimaye alifanikiwa kutengeneza saruji baada ya majaribio chungu nzima.  ***

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Muhammad Ali Shah Qajar aliomba hifadhi katika ubalozi wa Russia mjini Tehran.

Kushika kasi na kupanuka wigo wa cheche za Mapinduzi ya Katiba (Constitutional Revolution) katika maeneo mbalimbali ya Iran kulipelekea kuibuka harakati ya kuikomboa Tehran ya wapigania katiba na wakafanikiwa kupata ushindi.

Vikosi vya Muhammad Ali Shah Qajar vilishindwa jirani na mji wa Tehran. Hatimaye mji wa Tehran ukadhibitiwa na wapigania Katiba. Muhammad Ali Shah Qajar baada ya kuona kuwa amezidiwa nguvu na wanaharakati hao alikimbilia katika ubalozi wa Russia na kuomba hifadhi.

Siku hiyo hiyo kukafanyika kikao cha dharura na Muhammad Ali Shah Qajar akauzuliwa na badala yake mwanawe Ahmad Mirza aliyekuwa na miaka 11 akatangazwa kuwa mfalme.

Muhammad Ali Shah Qajar

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi.

Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo. 

Umoja wa Mataifa

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elekroniki.

Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine.