Alkhamisi, tarehe 11 Januari, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Jamadithani 1445 Hijria sawa na 11 Januari 2024.
Miaka 12 iliyopita katika siku kama hii ya leo msomi wa nyuklia wa Iran, Mustafa Ahmad Roshan aliuawa shahidi na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Ahmad Roshan alikuwa msomi wa nne wa nyuklia wa Iran kuuawa na magaidi wa Israel na washirika wake. Mbali na kujishughulisha na masuala ya nyuklia msomi huyo alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya elimu na sayansi. Ahmad Roshan aliuawa yeye na dereva wake mjini Tehran akiwa njiani kueleka kazini kwake. Siku kadhaa baadaye genge la magaidi waliomuua msomi huyo wa nyuklia wa Iran na wenzake lilitiwa nguvuni na wanachama wake wakakiri kuwa wana uhusiano na utawala haramu wa Israel na kwamba walipewa mafunzo na maajenti wa utawala huo haramu kwa ajili ya kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita sawa na tarehe 11 Januari mwaka 1992, Rais Shazli bin Jadid wa Algeria alijiuzulu baada ya Harakati ya Uokovu wa Kiislamu ya Algeria (FIS) kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa na matukio ya baadaye nchini humo. Rais Shazli alichaguliwa kuwa rais wa Algeria mwaka 1979 baada ya kifo cha Houari Boumediene, rais wa zamani wa nchi hiyo. Mwaka 1988 Shazli bin Jadid aliahidi kutekeleza marekebisho na kufanya mabadiliko ya katiba ya Algeria, ambapo kwa mujibu wake suala hilo lingetoa mwanya wa kutambuliwa rasmi vyama vya kisiasa.
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita aliaga dunia Ustadh Abulqassim Sahab, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya jiografia na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria Shamsiya katika mji wa Tafresh nchini Iran. Abulqassim Sahab alijifunza fiqih na usul kwa maulamaa wa mji huo na mbali na kupata elimu hiyo alizungumza pia lugha za Kiingereza na Kijerumani.
Miaka 143 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alimu na mtaalamu wa fasihi wa Kiirani, Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani. Mbali na kubobea katika elimu ya fiq'hi, Tankabani pia alikuwa mtaalamu katika fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake. Muhammad bin Suleiman ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na "Al Fawaidu fii Usuliddin" na " Qisasul-Ulama." Katika kitabu hicho kilichochapishwa mara kadhaa nchini Iran alizungumzia maisha ya maulama wa kabla yake.

Siku kama ya leo miaka 699 iliyopita mji wa Mexico ambao hivi sasa ni mji mkuu wa nchi ya Mexico, uliasisiwa na mmoja wa wafalme wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa miongoni mwa makabila ya Wahindi Wekundu wa Amerika ya Latini ambao waliwasili huko Mexico katika karne ya 12 na kutawala eneo hilo mwanzoni mwa karne hiyo.
Katika siku kama hii ya leo na miaka 855 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatibi, msomi mashuhuri wa Qur'ani aliyekuwa maarufu kwa jina la Imamul Qurra. Abul-Qasim alizaliwa mwaka 538 Hijiria. Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika taaluma ya usomaji wa Qur'ani, alikuwa pia mtaalamu wa elimu ya tajweed, tafsiri ya Qur'an, hadithi, sarufi ya lugha ya Kiarabu na elimu nyinginezo za kipindi hicho. Licha ya kuwa kipofu lakini alisifika kwa kuwa hodari na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani mwake. Msomi huyo wa Kiislamu ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kiitwacho "al Qasidatus Shatwibiyyah" kilichokusanya masuala yanayohusiana na elimu ya tajweed.
