Jumamosi, 13 Januari, 2024
Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Rajab 1445 Hijria sawa na tarehe 13 Januari 2024 Miladia.
Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab. ***

Siku kama ya leo miaka 1388 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. ***

Tarehe 13 Januari miaka 574 iliyopita alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno kwa jina la Bartholomew Diaz. Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz aligundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika. Miaka kumi baadaye baharia mwenzake kwa jina la Vasco Da Gama naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo. ***
Siku kama ya leo miaka 333 iliyopita aliaga dunia George Fox mwanamageuzi wa Kikristo wa nchini Uingereza. Fox alizaliwa 1624 katika familia ya kidini. George Fox alishindwa kustahamili mgongano uliokuwako katika maneno na vitendo vya makasisi na wafuasi wa Ukristo na vilevile vita vya watawala wa zama hizo. Akiwa na umri wa miaka 19, Fox alikata shauri kufanya utafiti kwa ajili ya kutafuta ukweli. George Fox alikuwa akiamini kwamba, kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho asili ya Ukristo na kujiepusha na umwagaji damu na wakati huo huo kusimama kidete kukabiliana na dhulma. Hata hivyo, Fox nae pia alitumbukia katika makosa kwenye itikadi zake. Pamoja na hayo, fikra zake zilipingana na mafundisho ya Ukristo katika zama hizo. Mara kadhaa George Fox alitiwa mbaroni na kutupwa jela na mamia ya wafuasi wake walikuwa wakiteswa gerezani. Harakati yake ya kupigania mabadiliko ya kidini iliendelea baada ya kuaga kwake dunia na harakati hiyo ingalipo. ***
Miaka 83 iliyopita katika siku kama hii mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza. Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia. Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo. Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakitaka kurejea Tehran Imam Khomeini (ra), kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo la kinyama ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath, likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti, lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi ya raia na wapiganaji wa Iran katikakipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 walijeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku. ***