Jan 17, 2024 23:33 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 18 Januari, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Rajab 1445 Hijria sawa na 18 Januari mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 962 iliyopita Hassan Sabbah mmoja wa viongozi wakubwa wa Waislamu wa Shia Ismailiya, alitwaa udhibiti wa ngome muhimu na imara ya Alamut, iliyo karibu na mji wa Qazvin, kaskazini mwa Iran.

Hassan Sabbah ambaye kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hapo alikuwa akiwalingania watu kumfuata yeye, aliimarisha utawala wake baada ya kutwaa udhibiti wa ngome hiyo na muda mfupi baadaye alidhibiti miji mingine.

Baada ya kudhibiti ngome hiyo ya Alamut, kuliongezeka tabligh (linganio) za kuwataka watu wajiunge na madhehebu ya Shia Ismailiya na wafuasi wa wake walifanya mauaji dhidi ya viongozi wa utawala wa Seljuqi, akiwemo Khoja Nidham al-Mulk. Ngome ya Alamut iliendelea kuwa tegemeo la wafuasi wa Ismailiya nchini Iran hadi pale ilipoangukia mikononi mwa utawala wa Hulagu Khan mwaka 654 Hijiria. Hassan Sabbah alifariki dunia mwaka 518 Hijiria. 

Hassan Sabbah

Tarehe 6 Rajab miaka 929 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq.

Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima. 

Siku kama ya leo miaka 335 iliyopita alizaliwa mwandishi na mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa, Charles de Montesquieu.

Alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. 

Kitabu maarufu zaidi cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva.

Katika kitabu hicho alichunguza aina mbalimbali za serikali zilizojitokeza katika kipindi chote cha historia, ada na sheria za kimaumbile, sheria za kibinadamu na uhusiano baina yao. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni "Persian Letters" (Barua za Kiiran). Alifariki dunia mwaka 1755.   

Charles de Montesquieu

Tarehe 18 Januari miaka 109 iliyopita 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Lengo kuu la mtakaba huo lilikuwa ni suala la kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean. 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani.

Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo.

Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa. 

Georges Clémenceau