Jumamosi, 20 Januari, 2024
Leo ni Jumamosi tarehe 8 ya mwezi Rajab 1445 Hijriai mwafaka na tarehe 20 Januari 2024 Miladia
Siku kama ya leo mwezi 8 Rajab, yaani miaka 412 iliyopita kwa mujibu wa kalenda na Hijria, alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa zama hizo hususan katika elimu za fiqhi na Hadithi. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwake ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Ummah. Mwanazuoni huyo aliaga dunia mwaka 1114 Hijria. ***

Miaka 124 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia John Ruskin mwandishi, mwanafalsafa na mkosoaji mashuhuri wa Uingereza. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Ruskin alizaliwa mwaka 1819 mjini London. Awali Ruskin alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi. Malenga huyo wa Uingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "modern painters". ***
Tarehe 20 Januari miaka 104 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life". ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi. Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. ***
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu. ***
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita sawa na tarehe 30 Dei 1357 Hijria Shamsia, Mhandisi Mehdi Bazargan, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifariki dunia. Mhandisi Bazargan alizaliwa mjini Tehran na kuhitimu masomo yake ya uhandisi wa magari huko nchini Ufaransa. Alikuwa mhadhiri pia katika Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika harakati za kisiasa wakati wa kujiri tukio la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Muda mchache kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Mehdi Bazargan alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na kwa pendekezo la baraza hilo alitakiwa kuunda serikali ya muda. Hata hivyo serikali yake ilidumu kwa muda wa miezi 9 tu kutokana na kuwa na tofauti za kimsingi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupenya katika serikali hiyo vibaraka waliokuwa dhidi ya mapinduzi. Hatimaye Bazargan aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua maradhi ya moyo.***