Jan 20, 2024 23:06 UTC
  • Jumapili, 21 Januari, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 9 ya mwezi Rajab 1445 Hijria mwafaka na tarehe 21 Januari 2024 Miladiia.

Siku kama hii ya leo miaka 482 iliyopita aliuawa shahidi Izuddin Sayyid Hussein, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa karne ya 10 Hijria. Alizaliwa mwaka wa 906 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil huko Lebanon na kujifunza elimu za wakati huo na kupata nafasi za juu za kielimu. Watu wenye chuki na husda, ambao hawakuweza kuvumilia utu na shakhsia yake kubwa ya kiroho na kidini katika mji wa Sayda (Sidon) huko Lebanon, walimpa sumu mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu na kumuua katika siku kama hii ya leo. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 288 iliyopita tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo. Ghuba ya Bengali iko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali. ***

Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita Mfalme Louis XVI wa Ufaransa alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XVI kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyongwa. ***

Mfalme Louis XVI

 

Siku kama ya leo miaka 45 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. ***

Imam Khomeini

 

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, mamluki wa utawala wa kidikteta wa Shah nchini Iran walishambulia Chuo Kikuu na Tehran na na kuwajeruhi wanafunzi wengi. Wanachuo hao walikuwa wakiandamana kudai haki za wanafunzi waliokuwa wameandamana na kisha kukabiliwa na vitendo vya kikatili vya maafisa usalama. Askari hao waliwapiga vibaya makumi ya wanachuo na wahadhiri na kuharibu nyenzo za masomo kama vitabu na maabara. Baada ya tukio hilo, serikali ya wakati huo kwa kuhofia kuenea malalamiko ilikifunga Chuo Kikuu cha Tehran kkwa muda wa miezi miwili na nusu. ***

Chuo Kikuu cha Tehran