Jan 24, 2024 23:24 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 25 Januari, 2024

Leo ni Akhamisi tarehe 13 Rajab 1445 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 25 Januari 2024.

Leo tarehe 13 Rajab zinaanza siku zinazojulikana katika dini kuwa ni "Siku Nyeupe" au siku za ibada ya Itikafu ambazo ni siku za tarehe 13, 14 na 15 za mwezi huu wa Rajab.

Katika siku hizi waumini wanashauriwa kufanya ibada ya itikafu ya kukaa na kubaki katika sehemu au mahala maalumu hususan misikitini na maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu SW. Watu wanaofanya itikafu hutakiwa kufunga Saumu siku tatu mfululizo wakiwa katika jitihada za kuondoka katika minyororo ya dunia hii finyu na kujikuribisha kwa Allah.

Ibada ya itikafu imehimizwa sana na Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake.

Siku kama ya leo miaka 1468 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib.

Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW.

Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.

Katika siku kama ya leo miaka 568 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg.

Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'

Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho.   

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen.

Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto.

Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani. 

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Tarehe 5 Bahman miaka 45 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji. Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran.

Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah. Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.  ***

Siku  kama ya leo miaka 18 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo.

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.