Alkhamisi, Februari 8, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Rajab 1445 Hijria sawa na Februari 8 mwaka 2024 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1458 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu.
Kipindi hicho Mtume Muhammad (saw) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (saw) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alitumia muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa.
Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumwambia kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake wa Mwisho kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanaadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Siku kama ya leo miaka 978 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari.
Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za Hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha.
Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".
Katika siku kama ya leo miaka 216 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia.
Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum.
Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Katika siku kama hii ya leo miaka 61 iliyopita Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa jeshi wa Chama cha Baath.
Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo.
Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq.
Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah.
Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakijibu wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi.
Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran waliokuwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini. Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani.
Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.