Feb 13, 2024 23:03 UTC
  • Jumatano, Februari 14, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 4 Sha'ban, 1445 Hijria, sawa na tarehe 14 Februari 2024 Milaadia

Siku kama ya leo miaka 1419 iliyopita, yaani tarehe 4 Sha'ban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas Bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl.

Mama yake ni Ummul-Banin, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa Mashahidi kiasi kwamba alisabilia katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi wamrejee kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu.

Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran.

Kwa mnasaba huu, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1005 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83.

Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria.

Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi. 

Kaburi la Abu Said Abul-Khayr

Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni waliokuwa na silaha na wanachama wa kundi la kigaidi la Palmach waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza shambulizi la kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati.   

Mauaji ya watu wa kijiji cha Sa'sa'

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita sawa na tarehe 14 Februari mwaka 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya Ujerumani.

Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa katika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu.

Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.   

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Martin Scott tabibu mpasuaji wa Uingereza alifanikiwa kuunganisha figo ya mwanadamu. Siku hiyo Prf. Scott alichukua figo ya mtu aliyekuwa amefariki dunia na kuiunganisha kwa mafanikio na mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika hospitali moja ya Leeds huko Uingereza. ****

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie, mwandishi wa kitabu cha "Aya za Shetani" au Satanic Verses kuwa ameritadi na kuondoka katika dini ya Kiislamu.

Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi.

Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fatuwa hiyo ya Imam iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Salman Rushdie

Katika siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61. Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004. 

Rafiq Hariri

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, ilianza harakati ya kupigania uhuru ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kiimla wa Aal-Khalifah.

Tangu Bahrain ilipopata uhuru mnamo mwaka 1971, wananchi wa nchi nchi hiyo wamekuwa wakitaka uhuru na demokrasia ambavyo vimekuwa vikikandamizwa na utawala huo. Tangu wakati huo, Waislamu wa Kishia ambao ndio wanaounda asilimia kubwa ya raia wa nchi hiyo, wamekuwa wakibaguliwa, kukandamizwa na kunyimwa haki zao za kimsingi.

Ni kutokana na hali hiyo ndio maana kwa mara kadhaa harakati hizo za kupigania uhuru zikawa zinaibuka dhidi ya utawala huo wa Aal-Khalifah ambao una mafungamano na Saudi Arabia ya Kiwahabi huku ukiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata hivyo badala ya utawala huo kusikiliza matakwa ya wananchi umekuwa ukitumia mtutu wa bunduki na ukandamizaji wa kuchupa mipaka katika kuzima harakati hizo.