Feb 20, 2024 22:47 UTC
  • Jumatano, tarehe 21 Februari, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 11 Sha'ban 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Februari 2024.

Siku kama ya leo miaka 1412 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake, Mtume Mtukufu (saw), alinufaika na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake, Imam Ali (as), na baba yake, Imam Hussein (as). Ali bin Hussein alikuwa maarufu kwa jina la Ali al Akbar yaani Ali Mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma za utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana.

Siku kama ya leo miaka 916 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.

Sanai Ghaznawi

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia aliyekuwa raia wa Uholanzi.

Dozy alizama katika taaluma za historia na lugha na kupata shabada ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusoma ytamaduni wa Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu.

Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Uislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania.

Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya Kisiasa na Tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu Kuanzia Mwanzo Hadi Katikati ya Karne ya 19' na 'Tamaduni za Mavazi ya Kiislamu.'

Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883. 

Reinhart Dozy

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Agha Najafi Isfahani, mmoja wa maulama wachaji-Mungu wakubwa na mwanamapambano. Alizaliwa mwaka 1262 Hijiri mjini Isfahan, Iran. Baba na babu yake, walikuwa kati ya maulama wakubwa wa eneo ambapo naye pia alipata kusoma kutoka kwao elimu mbalimbali. Baada ya Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani kusoma baadhi ya masomo ya kidini kutoka kwa baba yake (yaani Muhammad Baqir Agha Najafi) alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo mjini hapo. Miaka mitano baadaye alirejea mjini Isfahan na kuwa mmoja wa maraajii wakubwa wa mji huo. Aidha mbali na masuala ya kidini, Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani alikuwa mwanaharakati mzuri wa masuala ya kisiasa. Katika uwanja huo, msomi huyo alipambana vikali na upotoshaji wa kifikra na kiutamaduni na kadhalika ufisadi wa watawala dhalimu wa wakati huo. Wakati huo huo aliongoza harakati za kimapambano dhidi ya ukoloni wa kigeni hususan Uingereza. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Fiqhul-Imaamiyyah' 'Bahth Fii Wilaayati Haakimul-Faqih' na 'Dalaailul-Ahkam.'

Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia. 

Vita vya Verdun

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.   

Katika siku kama ya leo mia 59 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo.

Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.

Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Malcolm X

Tarehe 21 Februari miaka 51 iliyopita ndege ya abiria ya shirika la ndege la Libya iliyokuwa ikielekea Misri ilidunguliwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ndege hiyo ya raia ilikuwa njiani kutoka Tripoli, mji mkuu wa Libya, kuelekea Cairo, mji mkuu wa Misri, ilipopoteza njia kutokana na hali mbaya ya hewa na kuonekana kwenye jangwa la Sinai kaskazini mwa Misri.

Wakati huo, eneo la Sinai lilikuwa linakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, na ndege za kijeshi za utawala huo ziliishambulia bila kujali kwamba ndege hiyo ya Libya ilikuwa ya abiria. Abiria 108 kati ya 113 waliokuwemo kwenye ndege hiyo waliuawa.

Uhalifu huu uliamsha hasira ya walimwengu na ulilaaniwa piia na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO). ***

Na miaka 24 iliyopita kwa mara ya kwanza "Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama" iliadhimishwa. Uamuzi wa kuitangaza siku hii kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ulichukuliwa Novemba 1999 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo mwaka 2008 ulipewa pia jina la 'Mwaka wa Kimataifa wa Lugha". Sisitizo la kulinda na kuimarisha lugha ya mama linatokana na kuwa, takribani nusu ya lugha 6,000 zinazotambulika duniani zimo katika hatari ya kutokomea kutokana na sababu mbalimbali hususan uingiaji na utwishaji wa lugha za kimataifa kwa kutumia mbinu mbalimbali.