Jumatatu, tarehe 26 Februari, 2024
Leo ni Jumatatu 16 ya Sha'ban 1445 Hijria mwafaka na 26 Februari 2024.
Tarehe 26 Februari miaka 222 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo.
Hugo alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25.
Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani.
Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki mwaka 1885.

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia, mvumbuzi wa Marekani kwa jina la Richard Jordan Gatling.
Getling alizaliwa mwaka 1818 na katika umri wake alivumbua vitu kadhaa moja wapo ikiwa ni bunduki iliyopewa jina lake ya Getling.
Bunduki ya Getling ina mabomba kadhaa ambayo baada ya ufyatuaji kila moja huzunguka na kuachia risasi kwa hatua, na kuipa uwezo wa kufyatua risasi nyingi kwa wakati mmoja. Mzunguko wa mabomba hayo ulitengenezwa na Richard Jordan Gatling mwenyewe.
Miaka 68 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda.
Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5.
Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda.
Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita sawa na tarehe 7 Isfand 1377 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji ulifanyika katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa muktadha huo kukawa kumefikiwa moja ya lengo jingine miongoni mwa malengo matukufu ya taifa la Kiislamu la Iran.
Kwa kufanyika uchaguzi huo kwa hamasa, asasi na ngome ya wananchi ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji katika uga wa kiutawala ikawa imepata dhihirisho la kivitendo.
Kuundwa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji zaidi ya 33,000 katika maeneo mbalimbali ya Iran, ikawa ni hatua moja mbele katika uga wa kuingia na kuweko ushiriki wa wazi wa wananchi wote katika uchukuaji maamuzi ya nchi.
