Mar 01, 2024 08:05 UTC
  • Tuujue Uislamu (9)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Katika sehemu ya 9 ya mfululizo huu juma hili, tutaendelea kujadili maudhui ya Tawhidi yaani kuamini juu ya uwepo wa Mungu mmoja katika ishara zake katika alivyoviumba. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa wiki hii. Karibuni.

 

Ulimwengu wa uumbaji ni mkusanyo wa maajabu, na tunapotazama maajabu haya, tunahisi ukuu na adhama ya Muumba na kile ambacho si katika yeye kwa uoni na mtazamo wetu kinaonekana kuwa ni kidogo na dhalili. Kwa bahati nzuri, hii leo, kwa kupiga hatua elimu na kupatikana maendeleo ya elimu na ugunduzi wa baadhi ya siri za ulimwengu, milango ya teolojia na kumtambua Mungu imefunguliwa kwa wanadamu kiasi kwamba, tunaweza kusema kwa ujasiri kabisa  kwamba vitabu vya sayansi ya asili na mafundisho ya vitabu hivi yamejaa masomo ya kumtambua Mwenyezi Mungu.

Mtazamo wetu wa kuuliza na kudadisi juu ya uwepo ni ukumbusho wa kupata ukweli kwamba, uumbaji wa ulimwengu na muundo wake wa asili na wa kipekee ni kitabu kikubwa ambacho kila neno lake ni uthibitisho wa wazi wa uwepo wa Muumba wa ulimwengu. Sisi pia tunafungua kurasa za kitabu hiki na kuona maarifa, nguvu na hekima ya Mungu katika kurasa zake. Hapana shaka kuwa, katika kipindi chote cha historia, kutazama mbingu na dunia na matukio ya asili daima limekuwa jambo la kuvutia na la kutafakari kwa wanadamu. Kadiri wigo wa maarifa ya mwanadamu unavyozidi kupanuka huku pazia la siri za ulimwengu likiondolewa, ndivyo ukuu na adhama ya uwepo unavyoonekana zaidi, na kiu ya wanasayansi ya kupata habari mpya kuongezeka. Tangu mwanzo, mwanadamu amekabiliwa na maswali kuhusu anga na nyota; nini kinachotokea angani? Je, nyota, sayari na vingine vilivyomo mbinguni huwekwaje katika uzuri na utaratibu huo katika anga isiyo na mwisho? Je, kuna viumbe wanaoishi kwenye katika sayari zingine?

Kwa kutumia vifaa vya hali ya juu vya unajimu, wanadamu wamegundua kundi la sayari angani, ambazo kila moja ina mamilioni ya nyota.

 

Umbali kati ya Jua na Dunia yetu ni takriban kilomita milioni 150. Umbali huu unaitwa "kizio astronomia" Sayari ya mbali zaidi ni Neptuni ambayo ipo katika umbali wa vizio astronomia 30 kutoka Jua yaani ipo mara 30 mbali zaidi kutoka Jua kuliko Dunia. Pamoja na sayari kuna idadi kubwa ya violwa vingine. Violwa ni jina la jumla kwa ajili ya vitu vinayopatikana katika anga ya ulimwengu. Vingi ni vipande vidogo vya mwamba vinavyokusanyika katika kanda 3 zenye umbo la mwiringo.

Sayari hupatikana katika vikundi viwili. Mara nyingi zinaitwa "Sayari za ndani" na "Sayari za nje". Sayari nne za ndani ni Utaridi, Zuhura, Dunia na Mirihi ambazo ni ndogo na ni sayari za mwamba kama Dunia.

Katika miaka iliyopita wanaastronomia wamejadili uwezekano wa kuwepo kwa sayari za ziada katika umbali mkubwa. Imetambuliwa ya kwamba muundo wa mfumo wa jua ni mkubwa kuliko wataalamu wa kale walivyofikiri. Pamoja na maendeleo yote ya kisayansi na kiteknolojia, wanadamu wangali katika hatua za mwanzo katika uwanja wa kufikia siri za uwepo.

Kwa hivyo, siri nyingi za ulimwengu bado hazitambuliwi na mwanadamu. Tukiangalia mpangilio wa yote hayo kuanzia mbingu, nyota, sayari na vinginevyo ambavyo vimekuwa vikigunduliwa na wanasayansi siku baada ya siku, tunafikia natija hii kwamba, haya yote hayawezi kuwa yamejitokeza yenyewe bila ya kuweko aliyeyaleta na ambaye anasimia uendeshaji wake ambao kwa hakika una nidhamu na mpangilio wa hali ya juu.

 

Anga ya kushangaza ambayo iko juu yetu na maelfu ya nyota huangaza ndani yake usiku, hufanya moyo wa mwanadamu mwenye kutafakari kumuelekea muumba wa ulimwengu au kwa akali kujiuliza aliyevileta hivi. Tunasoma katika Surat Yasin  kuanzia Aya ya 36 hadi ya 40  kwamba:

Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyomea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani. Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.

Je umewahi kufikiria kuhusiana na uvutano wa dunia? nguvu mvutano na graviti ni kani ya kuvutana iliyopo kati ya maada yote ya ulimwengu. Kila gimba lenye tungamo linavuta magimba mengine yote yenye tungamo. Ndiyo sababu watu wanatembea ardhini ilhali hawawezi kuelea hewani: kwa sababu tungamo ya dunia inawavuta kuelekea kiini chake.  Nidhamu na mpangilio wa namna hii kwa hakika hakiwezi kuwa ni kitu kilichotokea chenyewe na kinachojiendesha bila ya usimamizi madhubuti.

Tukirejea katika Qur’an tunaona kuwa Aya ya pili ya tatu za Surat Raad zinasema: Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona, ametawala kwenye Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi. Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.

Aidha Aya ya 10 na 11 za Surat Luqman zinaashiria Muumba wa vilivyomo ulimwenguni na kutoa changamamoto ya kuonyeshwa wameumba nini wasiokuwa Yeye. Aya hizo zinasema:

Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri.

 

Wapenzi wasikilizajhi muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati tukutane tena juma lijalo. Kwaherini.