Jumamosi, 02 Machi, 2024
Leo ni Jumamosi 21 Shaaban 1445 Hijria sawa na tarehe Pili Machi 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita sawa na tarehe Pili Machi mwaka 1896 mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua nururishi. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia. ***
Miaka 68 iliyopita katika siku kama hii, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterrania na Bahari ya Antlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Morocco ilikombolewa na Waislamu mwishoni mwa karne ya Saba Miladia na silsila kadhaa za kifalme zilitawala nchini humo. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1956. ***
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika shughuli ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq. Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo. Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003. ***

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya vikosi vya dikteta Saddam kushindwa mtawalia katika medani ya vita, utawala wake uliamua kubadilisha mahesabu ya vita kwa maslahi yake na hivyo kuanza kushambulia kwa mabomu na makombora miji na kulenga meli za mafuta. Baadaye Iraq ikatangaza wazi kwamba, itashambulia kijeshi maeneo ya raia. Mashambulio hayo yaliyotekelezwa kwa lengo la kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran na matokeo yake ni kupanua wigo wa vita, yalionyesha kushindwa na kugonga mwamba mikakati ya kijeshi ya Iraq katika kuivamia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.