Jumapili, 3 Machi, 2024
Leo ni Jumapili 22 Shaaban 1445 Hijria mwafaka na 3 Machi 2024 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 857 iliyopita alifariki dunia mfasiri, faqihi, mpokezi wa Hadithi na alimu mkubwa wa Kiislamu Ibn Shahrashub. Alizaliwa mwaka 489 katika mji wa Mazandarani ulioko kaskazini mwa Iran na kuaanza kutafuta elimu na maarifa katika kipindi cha ototoni. Bin Shahrashub alikuwa amekwishahifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 8. Alipata ruhusa ya kunukuu hadithi za Mtume (saw) kutoka maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Zamakhshari, Muhammad Ghazali na Khatib Khorazmi na alikuwa hodari katika kutunga mashairi. Moja ya mashairi yake ya kuvutia ni lile alilotunga akitaja sifa na matukufu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Shairi hilo linapatikana katika kitabu cha Manaqib Al Abi Twalib. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika elimu za hadithi na sayansi ya Qur'ani Tukufu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 672 iliyopita, Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba lifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria. ***

Miaka 321 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uiingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya utafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia. Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli. Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa. ***
Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan. ***

Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan. ***

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji hayo dhidi ya Waislamu. ***
