Jumatatu, 4 Machi, mwaka 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Sha'ban 1445 Hijria sawa na tarehe 4 Machi mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1141 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw).
lizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume SAW akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi.
Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi mjini Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu.
'Al-Bisat' 'Tafsir al-Atroosh' na 'Imamatul-Kabir' ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo.
Miaka 712 iliyopita na katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Hussein bin Abdullah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafuddin aliaga dunia.
Alikuwa mpokezi wa hadithi na na mwanafasihi mkubwa. Abdullah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika zama zake. Mwanazuoni huyo alikuwa akitilia mkazo suala la kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na Hadithi.
Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni 'Tafsirul-Qur'an' na 'Sherh al Meshkat'.

Miaka 628 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria.
Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Alikuwa na mapenzi na itikadi thabiti na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala.
Silsilat al-Dhahab na Baharestan ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami.
Tarehe 4 Machi miaka 201 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu elfu 12 wakati wa vita vyao dhidi ya jeshi la ufalme wa Othmania katika mji wa Tripolitsa.
Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya utawala wa Kiothmani yaliamua kulipiza kisasi kwa kuua kundi la Wagiriki.
Na siku kama ya leo miaka 54 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu na mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Iran. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni. Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu.
Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo.
Na Tarehe 4 Machi inajulikana kama Siku ya Kupambana na Unene Duniani (World Obesity Day) katika kalenda ya kimataifa.
Siku ya Unene Duniani, ambayo hadi 2020 iliadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka, ilianzishwa kwa ushirikiano wa Shirikisho la Unene Duniani ili kutoa masuluhisho ya vitendo ya kusaidia watu kufikia uzito wa afya, kupata matibabu sahihi na kushughulikia tatizo la unene. Siku hiyo pia huadhimishwa ili kuongeza ufahamu kuhusu magonjwa hatari zaidi yanayohusishwa na unene unaoathiri watu duniani kote.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha unene wa kupindukia kimeongezeka mara tatu tangu 1975 na kimeongezeka mara tano kwa watoto na vijana, na hali hii inaendelea katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Kwa sasa zaidi ya 35% ya idadi ya watu duniani wana unene wa kupindukia, na kama hali hii itaendelea, 50% ya idadi ya watu duniani itakuwa na unene wa aina hiyo ifikapo 2035.
Siku hii imeainisha ili kukumbusha tatizo hili na kutafuta njia za kurekebisha.
Lishe nzuri, mazoezi, kuweka malengo halisi, na ufuatiliaji wa uzito mara kwa mara ni miongoni mwa njia za kupambana na unene wa kupundukia.
