Alkhamisi, tarehe 7 Machi, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Sha'ban mwaka 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Machi mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1340 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo.
Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo.

Siku kama ya leo miaka 685 iliyopita, alifariki dunia Ibn Faswih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria.
Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifundisha elimu ya Hadithi na kufikia daraja za juu katika uwanja huo. Aidha msomi huyo mbali na elimu za dini, alisoma pia mashairi huku akiandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti ikiwemo fiqhi.

Katika siku kama ya leo miaka 750 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas.
Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli.
Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.
Tarehe 7 Machi miaka 259 iliyopita alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa sanaa ya upigaji picha.
Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833.
Siku kama hii ya leo miaka 88 iliyopita vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw, eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Mahdi Ruhani, faqihi na msomi mkubwa wa elimu ya theolojia ya Kiislamu.
Sayyid Mahdi Ruhani alizaliwa mjini Qum, Iran mwaka 1343 Hijiria. Akiwa kijana Sayyid Mahdi Ruhani alijifundisha elimu ya dini na alipofikisha umri wa miaka 20 akaelekea mjini Najaf, Iraq. Baada ya Ayatullah Sayyid Hossein Borujerdi kuwasili mjini Qum, Ayatullah Mahdi Ruhani alishiriki darsa zake na kusoma kwake elimu ya fiqhi na usulul fiqhi ambapo baada ya muda fulani alianza kufundisha masomo ya ngazi ya juu. Kadhalika Ayatullah Sayyid Mahdi Ruhani alifanya kazi kubwa ya kulinganisha vitabu vya mbinguni kama vile Taurati, Injili na Qur'an Tukufu kuhusu nukta shirikishi na zenye kutofautiana. Msomi huyo mtajika alikuwa alimu wa kwanza katika hauza ya kielimu ya Qum kuanza kufundisha elimu za umaksi na dialectic. Vilevile aliunga mkono harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini (MA).
Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni Firqatul Salafiyya, Buhuth Ma'a Ahlusunnah Wassalafiyyah na Ahadithu Ahlil Bait.
Ayatullah Sayyid Mahdi Ruhani alifariki dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 76 na kuzikwa karibu na Haram ya Bibi Fatimat Ma'asuma (as).