Mar 07, 2024 22:48 UTC
  • Ijumaa, tarehe 8 Machi, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Sha'ban 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Machi mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, aliuawa Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu.

Sayyid Jamaluddin mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin al Afghani, alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika taaluma za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi. Sayyid Jamaluddin Assadabadi alikuwa mmoja wa waanzilishi wa fikra ya umoja wa Kiislamu na mmoja wa wapinzani wakubwa wa ushawishi wa kikoloni katika nchi za Kiislamu. Alifanya jitihada kubwa za kuyaamsha mataifa ya Kiislamu kwa kuchapisha magazeti ya Al Urwatul Wuthqa mjini Paris na Dhiyaul  Khafiqin mjini London. Vilevile alieneza mawazo za kupigania uhuru miongoni mwa watu kwa hotuba zake za hamasa, na kwa sababu hiyo alikabiliwa na uadui na wakoloni na tawala dhalimu. 

Sayyid Jamaluddin Asadabad (Afghani)

Hatimaye, Sayyid Jamaluddin Asadabadi alikwenda kwenye mji mkuu wa utawala wa Kiothmania, Istanbul, baada ya kuandamwa na kufuatiliwa huko Ulaya. Hata hivyo Abdul Hamid, mfalme wa utawala huo alimpa sumu na kumuua shahidi. ***

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino.

Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino.

Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Ferdinand Marcos

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon. 

Leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke.

Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani.

Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake.

Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.