Jumapili, 10 Machi, 2024
Leo ni Jumapili 29 Shaaban 1445 Hijria ambayo inasadifiana na 10 Machi 2024.
Siku kama ya leo miaka 1226 iliyopita inayosadifiana na 29 Shaaban 219 Hijria, alifariki dunia Ibn Naeem mtaalamu wa elimu ya hadithi, faqihi na mpokezi wa riwaya za kihistoria. Msomi huyo alizaliwa nchini Iraq, na anahesabiwa kuwa mmoja wa wapokezi wenye itibari, mwenye kuheshimiwa na mwenye kuaminiwa kati ya maulamaa wa Kiislamu. ***

Siku kama hii ya leo miaka 1127 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir faqihi, mfasiri na mpokeaji hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza masomo ya fiqih na hadithi kwa wasomi watajika wa zama zake. Ibn Mundhir aliishi katika mji wa Makka hadi mwisho wa maisha yake baada ya kuwasili mjini humo kwa lengo la kuzidisha elimu na maarifa ya kidini. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu kadhaa akiwa Makka. Kitabu alichokipa jina la al Ashraaf ni moja ya vitabu vya msomi huyo ambacho ndani yake ameonyesha kipawa na elimu aliyokuwanayo katika taaluma ya hadithi. ***

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano. Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell. ***
Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita alifariki dunia Konstantin Ustinovich Chernenko, kiongozi wa zamani wa Urusi ya Zamani. Alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1911 Miladia katika familia ya kawaida na ya kijijini maeneo ya Siberia ambapo baada ya kuhitimu masomo yake na akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na idara ya vijana ya chama cha Ukomonisti, huku akiwa mwanachama rasmi miaka miwili baadaye. Kwa kipindi cha miaka 20 alikuwa mjumbe wa ngazi ya juu wa ofisi ya kisiasa wa chama cha Ukomonisti wa Urusi ya zamani na baada ya hapo akateuliwa kuwa katibu Mkuu. Aidha katika kipindi chote cha utawala wa Leonid Ilyich Brezhnev alikuwa akiandamana na Konstantin Ustinovich Chernenko na ni kwa ajili hiyo ndipo Wamagharibi wakamwita Chernenko kuwa ni kivuli cha Brezhnev. Baadaye alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo na kufanikiwa kuongoza kwa kipindi cha miezi 13 na kufariki dunia katika siku kama ya leo mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 74. Ni baada ya kufariki dunia ndipo akachaguliwa Mikhail Sergeyevich Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani. ***
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Haj Hussein Khadimi alizaliwa mjini Isfahani, Iran mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi. Akiwa na umri wa miaka 26 alifikia daraja ya ijtihadi ambapo baada ya kurejea mjini Isfahani alijikita na shughuli ya ufundishaji sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi ambapo alikuwa na wanafunzi wengi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake kutovaa hijabu Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran. ***