Jumatatu, 11 Machi, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 30 ya mwezi Sha'ban 1445 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 11 Machi 2024.
Siku kama ya leo miaka 1120 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu.
Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.
Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika Idara ya Siasa ya Chama cha Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko.
Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita yaani mwaka 2004, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa kufuatia miripuko 5 ya mabomu iliyotokea kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid, Uhispania.
Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia.
Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo iliituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika katika miripuko hiyo.
Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Socialist kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq.

Na miaka 13 iliopita katika siku kama ya leo yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa daraja 9 kwa kipimo cha Rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan.
Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa kwa watu elfu 12 na malaki kadhaa ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo halijawahi kutokea mfano wake tangu makumi ya miaka yaliyopita nchini humo. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda kadhaa Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi.
Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.