Hadithi ya Uongofu (43)
Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji unapokutana nami katika kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hujadili masuala mbalimbali ya kijamii, kidini, kimaadili na kadhalika na kunukuu hadithi za miongozo kuhusiana na maudhui hizo.
Moja ya sifa nzuri za kiutu na kibinadamu ni kulea mayatima na kuwaonyesha huba na mapenzi. Katika maisha ya wanadamu kawaida huweko mapengo na mapungufu ambayo kuyaondoa kwake huwezekana kupitia watu wakarimu na wenye kujitolea kusaidia wengine. Kuwalea mayatima na kuwaonesha huba na mapenzi ili wasihisi ombwe na upweke wa kutokuweko wazazi wao ni miongoni mwa amali hizo za kibinadamu. Hii ndio maudhui ya kipindi chetu kwa juma hili. Kuweni nami kutegea sikio sehemu ya 43 ya mfulizo huu. Karibuni.
Haja ya huba na hali ya kujaliwa ni jambo ambalo liko kwa kila mwanadamu na katika kipindi cha utoto haja hii ya kuhitajia kuonyeshwa huba na kuzingatiwa huhisika zaidi ambapo haja hii hukidhiwa na wazazi yaani baba na mama. Lakini watoto mayatima wamekosa neema hii. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana katika Uislamu suala la kumuonesha huba na mapenzi yatima kwa kumpangusa pangusha kichwani limetiliwa mkazo na kuusiwa mno. Katika aya ya 177 ya Surat al-Baqarah Mwenyezi Mungu anataja vielelezo na misdaqi za kutenda wema na analitaja suala la kumuonesha mapenzi yatima baada ya imani juu ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Malipo, kumuamini Mtume na vitabu vya mbinguni na Malaika. Aya hiyo inasema:
Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
Aidha Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume SAW katika Surat al-Dhuha kwamba:
Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi?
Mwenyezi Mungu anamtaka Mtume SAW awaoneshe mapenzi mayatima na asiwakimbie na kujitenga nao.
Mtume Muhammad SAW ambaye ndiye aliyeleta ujumbe wa rehma kwa walimwengu na ambaye yeye mwenyewe alionja machungu ya kuwa yatima udogoni anasema kuhusiana na ujira na malipo ya mtu anayewasimamia na kuwalea mayatima kwamba:
Mtu ambaye atamsimamia yatima mpaka yatima huyo atakapokuwa na uwezo na kutokuwa mhitaji, Mwenyezi Mungu atakufanya kuingia peponi kwa mtu huyo kuwa ni jambo la wajibu, kama ambavyo pia kama mtu atafanya hiana na usaliti katika mali ya yatima anastahiki kuingizwa katika moto wa Jahanamu."
Mtume SAW ambaye ni kiigizo na ruwaza njema kwetu, alikuwa mfano wa wazi na wa kivitendo katika kuwasimamia na kuwalea mayatima.
Inanukuliwa kwamba, siku moja Bwana Mtume SAW alikuwa akipita katika moja ya barabara kuu za Madina kisha akawaona watoto kadhaa wamemzunguka mtoto mmoja aliyekuwa akilia na walikuwa wakimdhihaki na wakimwambia, wewe huna baba lakini baba yetu sisi ni fulani bin fulani na hadhi na cheo chake ni fulani. Mtume SAW alisogea mpaka kwa yule mtoto yatima na akamuuliza. Kwa nini unalia? Mtoto yule akasema, mimi ni mtoto wa fulani ambaye aliuawa katika vita vya Uhud, mama yangu ameolewa na kunitelekeza mimi na nilikuwa na dada yangu pia ambaye naye amefariki dunia.
Mtume SAW alimkumbatia mtoto yule na kumuonesha huba na mapenzi ya hali ya juu na akamwambia:
Kama baba yako aliuawa mimi ni baba yako na mke wangu ni mama yako na Fatima binti yangu ni dada yako. Mtoto yule alifurahi mno na kupaza sauti akisema, nyinyi watoto sasa msinitanie tena, kwani baba, mama na dada yangu ni watu bora na wenye daraja ya juu kuliko nyinyi nyote.
Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, watu wanapaswa kuzungumza kwa maneno mazuri na upole wa hali ya juu na mayatima na wawalishe na kuwapatia mavazi kwa njia inayostahiki na kuwaenzi popote pale na katu haipaswi kuwafanyia maudhi, kuwadhulumu, kuwaonea na kuwanyanyasa. Katika hadithi pia suala la kuwafanyia ukarimu mayatima limesisitizwa na kutiliwa mkazo mno.
Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa; Nyumba bora kabisa ya Waislamu ni ile ambayo ndani yake anaishi yatima ambaye anatendewa wema na kufanyiwa muamala mzuri; na nyumba mbaya kabisa ni ile ambayo ndani yake yatima anavunjiwa heshima na kufanyiwa maudhi.
Aidha Imam Ali AS amesema, katika kuwaadabisha na kuwaadhibu mayatima kutokana na makosa, amialiane nao kama watoto wenu.
Inanukuliwa kutoka kwa mmoja wa masahaba wa Mtume SAW akisimulia kwa kusema:
Siku moja tulikuwa tumekaa pamoja na Bwana Mtume SAW, mara akaja mtoto wa kiume na kumwambia Mtume: Mimi ni mtoto yatima na nina dada yatima na mama yetu ni mjane. Tulishe katika kile alichokulisha Mwenyezi Mungu kiasi kwamba, Allah akupatie mpaka ufurahi. Mtume SAW akasema, umesema maneno mazuri mno ewe mtoto. Kisha Mtume akamwambia mmoja wa Masahaba zake aliyejulikana kwa jina la Bilal, nenda ukamletee kile tulichonacho. Bilal akaenda na kuleta tende 21 zilizokuwa ndani. Mtume SAW akasema: Tende saba ni zako, saba nyingine ni za dadako na saba zilizobakia ni za mama yako.
Muadh bin Jabal mmoja wa masahaba wa Mtume aliyekuwa amepambika kwa tabia njema na aliyekuwa mkarimu akasimama na akamgusa kichwani yatima yule kwa huba na mapenzi na kusema:
Mwenyezi Mungu afidie uyatima wako na akufanye kuwa mrithi mwema wa baba yako. Baada ya Mtume SAW kushuhudia kitendo hicho kizuri cha Muadh bin Jabal akamuuliza. Msukumo wa kitendo chako hicho ni nini? Muadh bin Jabal akasema: Kumuonyesha huba na upendo mtoto huyu. Kisha Mtume akasema: Ninaapa kwa yule ambaye kutolewa kwa roho yangu kuko katika uwezo wake, kila Mwislamu ambaye atachukua jukumu la kusimamia na kumlea yatima na kufanikiwa katika jukumu hilo, na akamuonyesha huba na mapenzi yatima kwa kumpangusa pangusha kichwani, kupitia kila unywele unaoguswa na mkono wake Mwenyezi Mungu atamuinua daraja moja, atamuandikia thawabu moja katika daftari la amali na kupunguziwa dhambi moja.
Ndio maana katika utamaduni wa Kiislamu ili kuweza kuondoa mapungufu wanayokabiliwa nayo watoto mayatima, mtu anapochukua jukumu la kumlea yatima anapaswa kumhesabu kuwa miongoni mwa wanawe.
Imam Muhammad Baqir AS anasema: Sifa nne kama zitatimia kwa mtu yeyote, basi Mwenyezi Mungu atamjengea nyumba mtu huyo peponi. Mtu ambaye amempa hifadhi yatima, mwenye kuonesha kuguswa na kumuonea huruma mtu asiyejiweza, akawaonesha huba na mapenzi baba na mama na akayafumbia macho baadhi ya makosa ya walio chini yake.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.