Mar 28, 2024 05:58 UTC
  • Jumatano, tarehe 27 Machi, mwaka 2024

Leo ni Jumatano tarehe 16 Ramadhani 1445 Hijria sawa na Machi 27 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 718 iliyopita, alifariki dunia Ibn Zamlakani, mtaalamu wa sharia za Kiislamu, hadithi na fasihi mkubwa wa mjini Damascus, Syria. 

Ibn Zamlakani alisoma elimu mbalimbali kutoka kwa maulama wakubwa wa zama zake huku akiipa umuhimu mkubwa elimu ya dini na hadithi. Miaka 20 baadaye Ibn Zamlakani alifikia daraja ya kutoa fatwa katika masuala ya dini. Alijishughulisha pia na shughuli za ukadhi na ukufunzi katika shule tofauti za mji wa Damascus.

Moja ya athari za Ibn Zamlakani ni pamoja na kitabu cha 'Burhanul-Kaashif an I'jaazil-Qur'an.'   

Siku kama ya leo miaka 600 iliyopita alifariki dunia Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu.

Maqrizi alizaliwa mjini Cairo, Misri na baadaye kusoma elimu ya Kiislamu katika miji tofauti ya nchi hiyo kama ambavyo pia alikuwa na uhodari katika elimu mbalimbali za Kiislamu. Kwa muda fulani alifanya kazi ya ukadhi mjini Cairo. Alipendelea sana historia huku akiandika vitabu tofauti katika uwanja huo.

Miongoni mwa athari za Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi ni pamoja na kitabu cha 'as-Suluuk Lima'arifatil-Muluuk' ambacho kinazungumzia historia.   

Siku kama ya leo miaka 527 iliyopita, alizaliwa Hans Holbein the Younger, mchoraji wa Ujerumani katika familia ya kisanii.

Younger alijifundisha sanaa ya uchoraji kutoka kwa baba yake aliyekuwa mashuhuri katika uwanja huo. Baada ya hapo alielekea nchini Uswisi na kuvisaidia vyombo vya usalama katika shughuli ya kuonyesha taswira za watu hususan wahalifu.

Baada ya muda, alielekea Uingereza na kuendelea na kazi yake hiyo na kupata umaarufu mkubwa. Hans Holbein the Younger alifariki dunia mwaka 1543.   

Hans Holbein the Younger

Siku kama ya leo miaka 179 iliyopita alizaliwa Wilhelm Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani.

Mwaka 1845 aligundua miale ya X na mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X.

Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa sababu hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika. 

Wilhelm Conrad Rontgen

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita inayosadifiana na 27 Machi 1948, serikali ya Ufaransa iliasisi jumuiya iliyozishirikisha Ufaransa na nchi waitifaki, pamoja na nchi ambazo zilikuwa makoloni ya nchi hiyo kwa kuzikutanisha pamoja nchi hizo. Muungano wa nchi hizo unafanana na ule wa Jumuiya ya Madola, ambao unazijumuisha nchi zilizowahi kutawaliwa na Uingereza. Kuundwa kwa muungano huo ulikuwa mwanzo wa kuandaliwa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa 'Francophonie' ambayo iliasisiwa mwaka 1970. Wanachama wengi wa jumuiya hiyo wanatoka barani Afrika. 

Miaka 56 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanaanga wa kwanza duniani Yuri Gagarin.

Baada ya kuhitimu masomo na kuchaguliwa katika klabu ya masuala ya anga ya Urusi ya zamani, Gagarin alijiunga na programu ya masuala ya anga ya Urusi ya zamani na kuteuliwa kati ya watu 20 waliotakiwa kufanya mazoezi ya kutumwa angani.

Tarehe 12 Aprili 1961 Yuri Gagarin alipanda kwenye roketi la Vostok 1 na kuwa mwanadamu wa kwanza kutumwa katika anga za mbali. Siku hiyo Gagarin aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89.

Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968. 

Yuri Gagarin