Jul 11, 2016 02:39 UTC
  • Jumatatu, Julai 11, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 6 Shawwal 1437 Hijria sawa na 11 Julai 2016.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina waliuawa kwa umati. Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wanamgambo wa Kiserbia wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade, waliuvamia mji wa Srebrenica licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitangaza eneo hilo kuwa la amani mwaka 1993 na kutumwa askari wa umoja huo katika mji huo. Waislamu wa mji wa Srebrenica walijaribu kuondoka katika mji huo, lakini watenda jinai wa Kiserbia waliwauwa wanaume na watoto wao wa kiume na kuwaruhusu wanawake kuondoka katika mji huo. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica.

Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17.

Miaka 459 iliyopita, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia.

Siku kama ya leo miaka 651 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokeaji wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Ba'labak moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhudi baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam.

Siku kama ya leo miaka 772 iliyopita, mji wa Baytul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Vita vya Msalaba vilifanyika kwa duru na awamu kadhaa.