Jumamosi, 30 Machi, 2024
Leo ni Jumamosi 19 ya mwezi mtuukufu wa Ramadhani 1445 Hijria mwafaka na 30 Machi 2024 Miladia.
Miaka 1405 iliyopita, katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Imam Ali bin Abi Talib (as) ambaye ni mkwe, binamu na mtu wa karibu sana kwa Mtume Muhammad SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya kichwani akiwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri katika Msikiti wa Kufa huko Iraq. Imam Ali alipigwa upanga na mtu aliyejulikana kwa jina la Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali (as) alikufa shahidi siku tatu baadaye. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili mkubwa katika Uislamu baada ya Mtume Muhammad (saw) na anaelezwa katika historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa wa kupigiwa mfano, mwenye imani thabiti, akhlaki njema, elimu na uadilifu usio na kifani. Alipata elimu na kulelewa katika nyumba ya Mtume Muhammad (saw), na alikuwa mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali (as) alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali (as) alikuwa mpole na mwenye upendo. Imam Ali daima alitetea haki na uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima, Imam Ali bin Abi Twalib anasema: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake." ***

Katika siku kama ya leo miaka 613 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ghiyathuddin Jamshid Kashani, mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. Alikuwa mwanahisabati na mnajimu mahiri sana. Ghiyathuddin alifanikiwa kuvumbua vifaa vingi vya lazima kwa ajili ya kuutazamia nyota. ***
Siku kama ya leo miaka 157 Russia iliiuzia serikali ya Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic. Russia iliiuza ardhi ya Alaska kwa Marekani kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ni jimbo la 49 la Marekani lenye ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, khususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki. ***

Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, maandamano makubwa ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kughusubu ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa. ***
