Jumapili, 31 Machi, 2024
Leo ni Jumapili mwezi 20 Ramadhani 1445 Hijria mwafaka na 31 Machi 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka wa 8 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka.
Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu.
Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi na kuwafanya waingie kwa wingi katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 903 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 542 Hijiria, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Kiislamu.
Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na ni kwa sababu hiyo ndio maana akaitwa al Alawi, al Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo.
Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamasah' na 'Mandhumat Ibn Shajari.' Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad, Iraq na kuzikwa mjini hapo. ***

Miaka 819 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 626 Hijiria, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na wasomi watajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria ambaye alikuwa mtaalamu mashuhuri wa jiografia.
Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru.
Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Mu'jamul-Buldan" na Mu'jamul- Udabaa." ***
Siku kama ya leo miaka 771 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ibn Saai Baghdadi, mtaalamu wa fasihi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu.
Sheikh Tajud-Din Abu Twalib Ali Ibn Anjub Ibn Uthman Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Saai, alizaliwa mwaka 593 huko Baghdad, Iraq. Alijifunza elimu za zama zake kwa walimu mbalimbali. Kwa miaka kadhaa Ibn Saai alisimamia maktaba ya utawala wa wakati huo mjini Baghdad ambayo ilitumiwa kwa ajili ya kutwalii. Baada ya Baghdad kudhibitiwa na silsila ya utawala wa Wamongoli, Ibn Saai Baghdadi aliteuliwa na Nasir al-Din al-Tusi kwa ajili ya kusimamia maktaba mbalimbali za mji huo. Ni katika kipindi hicho ndipo akatokea kuwa mwandishi mkubwa, jambo ambalo lilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha.
Kitabu cha 'al-Khulafaau' ni miongoni mwa athari mashuhuri za Ibn Saai. Vilevile ameandika kitabu cha 'Akhbarul-Udabaa' 'Akhbarul-Hallaj' na 'Akhbaru Qudhaatu Baghdad.' Abin Saai alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa Baghdad. ***

Miaka 428 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method. ***
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi, faqihi, mfasiri wa Qur'an Tukufu na hatibu mkubwa wa Iran. Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi alizaliwa mwaka 1309 Hijiria, mjini Qum na katika familia ya elimu na maarifa ya dini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alijiunga na masomo ya hawza kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kabir Qumi, Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi, huku akisoma pia elimu ya falsafa na theolojia kwa Ayatullah Mirza Ali Akbar Mudares Yazdi ambapo alifanikiwa kufikia ngazi ya juu ya kielimu. Alikuwa miongoni mwa shakhsia waliochangia katika uhamisho wa Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kutoka mjini Arak kwenda mjini Qum na hatimaye kuasisiwa hawza ya kielimu mjini hapo. Mbali na kubobea katika utafiti na kujibu shubuha mbalimbali za dini nyingine, alikuwa mjuzi katika masuala ya historia na jografia ya dini mbalimbali ambapo alitoa nadharia katika uwanja huo. Aidha maulama mbalimbali na maraaji walikuwa wakiheshimu nadharia zake hususan katika uga wa fiqhi huku Imamu Khomein (MA) akimpa lakabu ya 'Sheikh al-Twaifa'. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Risaalatu al-Dharar' 'Mantwiqul Hussein' na 'Maqswadul-Hussein.'
Tarehe 12 Farvardin miaka 45 iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kushiriki kwa wingi wananchi katika kura ya maoni, taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kihistoria wa kupasisha mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini. Zaidi ya asilimia 98 ya walioshiriki waliupigia kura ya ndiyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tarehe 12 Farvardin kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jamhuri ya Kiislamu. ***

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978. ***