Jumatatu, Aprili Mosi, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 21 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1445 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Aprili 2024 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita Ali bin Abi Talib AS, wasii wa Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa Ahlul Bait wa Mtume, aliuawa shahidi.
Siku mbili kabla ya kifo chake, Imam Ali bin Abi Twalib alipigwa upanga kichwani na mmoja wa wafuasi wa kundi la Khawarij wakati alipokuwa katika sijda ya Swala akimwabudu Mwenyezi Mungu msikitini. Siku kama ya leo Imam Ali (as) aliaga dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata na hivyo kufikia matarajio yake makubwa ambayo alikuwa akiyatamani daima, yaani kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu SW.
Kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) kulikuwa msiba mkubwa na usioweza kufidika kwa Uislamu na Waislamu.
Imam Ali (as) aliwausia wanawe na Waislamu akisema: "Nawausia kumcha Mungu na kuwa na taratibu nzuri katika mambo yenu. Wajalini yatima na muwafanyie mema majirani zenu, kwani nilimsikia Mtume wa Allah (saw) akiusia kuwafanyia mema jirani hadi nikadhani atawarithisha. Shikamaneni na Qur'ani na msiache watu wengine wawatangulie mbele katika kutekeleza mafundisho yake. Itukuzeni Swala kwani ndiyo nguzo ya dini yenu.." Sala na salamu za Allah jiwe juu ya Imam Ali bin Abi Twalib na Aali zake watoharifu. *

Tarehe 21 Ramadhani miaka 341 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Abu Ja'far Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon.
Alitokea kuwa miongoni mwa maulama na watafiti wakubwa wa Kiislamu. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na Hadithi, na miongoni mwa vitabu hivyo ni kile cha "Wasaailu al Shia" ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi.

Miaka 445 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.
Tarehe Mosi Aprili miaka 79 iliyopita vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan.
Mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege elfu 10 za kivita za Marekani zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa siku 83.
Hata hivyo Wajapani walipambana ipasavyo katika vita hivyo kwa ajili ya kulinda nchi yao kwa kadiri kwamba meli 36 za kivita za Marekani ziliharibiwa kikamilifu na nyingine 369 kutiwa hasara. Vilevile ndege za kivita 763 za Marekani zilitunguliwa.
Wajapan pia walipata hasara kubwa katika vita hivyo kwani wapiganaji laki moja na elfu kumi kati ya wapiganaji wote laki moja na elfu ishirini wa kisiwa cha Okinawa waliuawa au kujeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib A.S katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein A.S huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq.
Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait.
Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu.
