May 02, 2024 02:34 UTC
  • Alkhamisi, tarehe Pili Mei, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe Pili Mei 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 504 iliyopita, alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia, Leonardo da Vinci.

Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Baada ya kufanya safari katika miji kadhaa ya Italia, mwaka 1506 Da Vinci alielekea Ufaransa na kuwa mchoraji wa Mfalme Louis xii (12). Aliishi katika kipindi cha mchoraji mwingine mashuhuri wa Italia, Michelangelo, na wasanii hao wawili mashuhuri walitoa mchango mkubwa katika sanaa ya kipindi cha mwamko wa Ulaya (Renaissance). Miongoni mwa michoro maarufu ya Leonardo Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa".  Mbali na uchoraji, Leonardo Da Vinci alibobea pia katika taaluma nyingine kama hisabati.   

Leonardo Da Vinci

Katika siku kama ya leo miaka 333 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematullah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62.

Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu.

Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.   

Sayyid Neematullah Jazairi

Miaka 67 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Seneta wa chama cha Republican huko Marekani Joseph McCarthy.

Katika kipindi cha vita baridi McCarthy alikuwa kiongozi wa moja ya kamati za Baraza la Seneti la Marekani. Mwanasiasa huyo aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani akidai kwamba wanafanya ujasusi kwa maslahi ya Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilikuwa mwanzo wa harakati iliyopewa jina la McCarthyism ambayo kwa mujibu wake wasomi, wasanii na maafisa wengi serikalini walifuatiliwa na kuswekwa jela kwa kutuhumiwa kwamba wanafanya ujasusi kwa maslahi ya Urusi na kwamba wana fikra za kikomunisti.

Tume ya McCarthy ilifukuza maelfu ya wafanyakazi wa serikali na kuwasweka jela wasanii na waandishi wengi kwa tuhuma zisizo na msingi wowote. Miongoni mwa wasanii mashuhuri walioswekwa jela na tume hiyo ni Charlie Chaplin na Alfred Hitchcock.   *****

Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita Usama bin Laden kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda aliuawa na vikosi vya Marekani huko nchini Pakistan.

Usama aliyekuwa mmoja wa waasisi wa al-Qaeda alizaliwa Machi mwaka 1957 huko Riyadh nchini Saudi Arabia na kusoma katika Chuo Kikuu cha King Abdul-Aziz. Kundi la kigaidi la al-Qead linahusishwa na mauaji mengi duniani likiweko shambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 na mashambulio ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani Dar es Salaam Tanzania na Nairobi Kenya. 

Usama bin Laden