May 04, 2024 10:40 UTC
  • Tuujue Uislamu (16)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Kama mnavyojua, katika mfululizo wa mijadala tuliyokuwa nayo kuhusu imani juu ya Mungu Mmoja (tawhidi) na kumtambua Mwenyezi Mungu, tulifika kwenye maajabu ya uumbwaji wa mwanadamu. Tulisema Mwenyezi Mungu ametaja kuumbwa kwa mwanadamu katika Aya nyingi na ameutambulisha uumbaji wake wa asili pamoja na maajabu yake yote kwamba, ni katika ishara za tadibiri na uwezo wake. Wiki hii pia tutaendelea na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 16 ya mfululizo huu.

 

Mwenye Ezi Mungu ameumba ulimwengu kwa nidhamu na mfumo ambao hauwezi kufikiriwa kuwa mkamilifu zaidi kuliko huo. Mwenyezi Mungu anaashiria hili katika Aya ya 7 Surat al-Sajdah: Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo.

Bila shaka mnafahamu kwamba, moyo ni chombo na kiungo muhimu sana katika katika mwili wa mwanadamu na katika mzunguko wa damu. Ndiyo, moyo wa mwanadamu ni kiungo chenye misuli ambacho hupeleka damu kwenye sehemu zote za mwili kama pampu ya ajabu. Kwa ibara nyingine ya kitaalamu zaidi ni kwamba, Moyo ni ogani inayosukuma damu katika mishipa yake ambayo husafirisha damu kwenda sehemu zote za mwili ili ziweze kufanya kazi. Shughuli ya moyo ni ya masaa 24 bila kupumzika yaani usiku na mchana, hata wakati mtu amelala, moyo unaendelea kusafirisha damu na kupeleka katika viungo mbalimbali. Mfumo wa mzunguko wa damu ni jumla ya mishipa ya damu mwilini pamoja na moyo. Ni sehemu muhimu ya uhai wa viumbe wengi (lakini si wanyama wote).

Moyo hufunguka na kufunga zaidi ya mara 100,000 kwa muda wa saa 24 yaani siku moja inayoundwa na mchana na usiku. Moyo hupiga kwa mapigo yanayofuatana na yenye uwiano, yakiambatana na sauti ya mdundo. Kwa njia hii, wakati wa maisha ya miaka 70, hatua hii inarudiwa zaidi ya mara bilioni mbili na nusu.

Sasa tunapaswa kufikiria jinsi moyo unavyofanya kazi kwa usahihi na kwa muda mrefu, ambao una nguvu ya ajabu na kwa kazi hii yote na shughuli, hakuna usumbufu katika muundo na kazi yake! Ikiwa injini hii yenye nguvu katika mwili wa mwanadamu itasimama basi kifo hakitakuwa na shaka kwa mwanadamu huyu. Moyo ni moja ya viungo nyeti zaidi katika mwili.

 

Idadi ya mapigo ya moyo, mnyweo na upanuzi wake, ni tofauti katika umri tofauti. Hakika, ni hekima gani ya tofauti ya mapigo ya moyo katika umri tofauti? Hapa siri nyingine ya uumbaji inafichuliwa.

Tofauti hii inahusiana moja kwa moja na kiasi cha mahitaji muhimu ya mwili wa mwanadamu katika umri huu. Kwa maana kwamba, kadiri mahitaji muhimu ya seli za mwili yanavyokuwa mengi, ndivyo, kasi ya mzunguko wa damu na mapigo ya moyo huongezeka. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana, katika kipindi cha utotoni, wakati seli za mwili ni dhaifu, idadi ya mapigo ya moyo na kasi ya mzunguko wa damu ni ya juu.

Ikiwa tutafikiri kwa usahihi, tutapata kwamba, maendeleo ya mwanadamu katika nyanja yoyote ya kisayansi ni matokeo ya kazi ya maelfu ya wanasayansi katika uwanja huo. Ndivyo ilivyo katika sayansi ya matibabu. Yaani, kwa juhudi za madaktari na wapasuaji kwa karne nyingi, sayansi na elimu ya tiba ilikua polepole na kubadilika hadi mwanadamu akafikia hatua ambayo anaweza kuunganisha moyo wa mwanadamu na mwanadamu mwingine au kupandikiza moyo kwa lugha ya kitaalamu. Kwa tafsiri hii, inaweza kusemwa kuwa sayansi ya kisasa ya matibabu ni matokeo ya kazi ya wataalamu katika uwanja huu kwa maelfu ya miaka.

Ayatullah Makarem Shirazi, mwanazuoni, mwanafikra na mfasiri wa Qur'an, anaandika katika somo la teolojia na kumtambua Mungu:

Tunawezaje kuamini kwamba tunakuwa wasomi na wanasayansi kwa kuwa na ufahamu wa sayansi na maarifa tofauti, ambayo si chochote isipokuwa kujua sehemu tu sheri na mifumo ya ulimwengu, lakini kanuni ya kwanza, ambayo ni Muumbaji wa mifumo yote ya ulimwengu hana elimu na maarifa? Madaktari wa upasuaji wanaweza kupandikiza moyo wa mwanadamu kwa mwanadamu mwingine. Je! unaweza kuamini kuwa, wote walikuwa wanasayansi na wasomi, lakini yule ambaye alimuumba mwanadamu katika dunia hii, aliuweka moyo wake kifuani mwake na kuupandikiza kwenye mwili wake, na juu ya hapo akaufanya moyo kwa ajili yake, je, anakosa elimu na akili?! Mwisho wa kunukuu.

 

Wapenzi wasikilizaji hivi inawezekana kukubali kwamba, daktari bingwa wa upasuaji ni msomi na mwenye elimu na ujuzi, lakini aliyemuumba daktari huyu akawa hana elimu na maarifa? Bila shaka hilo ni jambo lisilokubalika kimantiki na kiakili pia.

Mfano mwingine wa maajabu miongoni mwa maajabu ya viungo vya mwanadamu ni macho.

Hivi umewahi kufikiria juu ya kazi ya kituo chako cha kuona, yaani jicho? Muundo wa macho ni ulimwengu wa maajabu. Jicho liko kichwani, yaani, nafasi ya juu kabisa ya mwili, ili mtu aweze kuwa na udhibiti zaidi ya yale yanayomzunguka. Jicho ni sehemu ya thamani zaidi ya mwili wa binadamu, ambayo iko ndani ya mashimo ya fuvu. Hali hii hufanya jicho kuwa salama iwezekanavyo kutokana na uharibifu. Jicho ni ogani inayotambua mwanga na kutuma habari zake kwa ubongo. Macho ya binadamu kama ya mamalia wengine huwa na lenzi moja tu. Lakini muundo wa jicho unaruhusu kuona rangi, umbali na mengi madogo. Mbali na macho viungo vingine kama ulimi, masikio na kadhalika navyo vinafanya kazi kwa umahiri na ustadi mkubwa na haiwezekani hili likawa ni jambo lisilo la muumba na msimamizi wake na umakini huu ni ishara ya wazi ya kuweko Muumba wa ulimwengu huu na vilivyomo akiwemo mwanadamu.

 

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki, sina budi kukomea hapa kwa leo. Msikose kujiunga name wiki iajyo katika sehemu nyingine ya Tuujue Uislamu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh