Ijumaa, tarehe 10 Mei, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Dhulqaada 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Mei mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1272 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kutegemewa, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan, huko kaskazini mashariki mwa Iran, kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario.
Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania.
Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya nchi hiyo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco.

Tarehe 10 Mei miaka 30 iliyopita yaani tarehe 10 Mei 1994, Nelson Rolihlahla Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya zaidi ya karne tatu za utawala wa makaburu wachache nchini humo.
Chama cha African National Congress (ANC) kilijipatia viti 252 kati ya jumla ya viti 400 vya Bunge la Afrika Kusini, kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na wa kihistoria nchini humo.
Baada ya kuchaguliwa, Rais Mandela alimteua Thabo Mbeki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na FW de Klerk kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Afrika Kusini.