Jumatatu, 13 Mei, 2024
Leo ni Jumatatu 4 Dhulqaada 1445 Hijria mwafaka na tarehe 13 Mei 2024.
Siku kama ya leo miaka 311 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa.
Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa.
Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanja tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765. ***
Katika siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Mei 1846, Kongresi ya marekani ilipasosha tangazo la vita dhidi ya Mexico.
Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas.
Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico. ***
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, Ayatullah Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu, katika hatua ya kukabiliana na ukoloni wa Uingereza, alitoa fatwa ya kuharamisha utumiaji tumbaku nchini Iran.
Katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar Uingereza ilikuwa ikiongeza satwa yake nchini Iran kwa kufungua makampuni ya tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini hapa.
Fatua hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika fatwa hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini. ****
Miaka 117 iliyopita katika kama ya leo, alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na thamthiliya wa Kiingereza.
Maurier alizaliwa katika familia ya wanasanaa na iliyokuwa pia na wanafasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi.
Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889. ***