Jumanne, tarehe 21 Mei, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Pili Dhulqaada 1445 Hijria mwafaka na tarehe 21 Mei 2024.
Tarehe Mosi Khordad mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ni siku ya kumuenzi Muḥammad Saddruddin Qawam Shirazi maarufu kama Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu.
Alizaliwa tarehe 9 Jamadil Ula mwaka 980 Hijria Qamaria huko Shiraz. Awali alielekea katika mji wa Qazvin ambao katika zama hizo ulikuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo kwa walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma fiqhi, usul, Hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Mulla Sadra alipa elimu kama sayansi asilia, hisabati, nujumu na nyota kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake.
Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 na kitabu cha al Asfar al-arba‘a ndio maarufu zaidi. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria huko Basra nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na akazikwa katika mji huo huo.
Siku kama ya leo miaka 2240 iliyopita, yaani tarehe 21 Mei mwaka 216 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), jeshi la mtawala wa Carthage chini ya uongozi wa Hannibal, lilishindwa vibaya huko kaskazini mwa Italia.
Hivyo vilikuwa vita vya pili baina ya utawala wa Carthage na Roma kwa anwani ya vita vya 'Punic.' Hannibal alishiriki vita hivyo kwa kutumia tembo na wapandaji tembo mahiri kabla ya kushindwa vibaya. ****
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, alizaliwa Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia.
Sakharov alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomeza silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975.
Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Sergeyevich Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo. ***
Miaka 44 iliyopita katika siku kama hii ya leo sawa na tarehe Mosi mwezi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsiya ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Marekani ambayo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran ilianza kuiwekea Iran mzingiro wa kiuchumi lengo likiwa ni kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na vilevile kuulazimisha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu kufanya mapatano na serikali ya Washington.
Baada ya uamuzi huo wa serikali ya Marekani; Imamu Khomeini (M.A) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kuwa uhai wa uchumi wa nchi mbalimbali hautegemei madola makubwa na kulihutubu taifa la Iran kuwa: Kamwe msiogope vikwazo vya kiuchumi; kama mtatuwekea mzingiro wa kiuchumi basi tutaimarika zaidi na ni kwa maslahi yetu."
Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India, aliuawa kigaidi.
Rajiv Gandhi alikuwa mwanawe Indira Gandhi Waziri Mkuu wa zamani pia wa nchi hiyo. Alizaliwa tarehe 20 Agosti 1944 mjini Bombay na kulelewa katika nyumba ya babu yake Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa kwanza wa India. Rajiv Gandhi aliingia katika ulingo wa siasa baada ya kuaga dunia mdogo wake ambaye alikuwa akitayarishwa kumrithi kisiasa mama yake Indira Gandhi. Alichukua hatamu za kuiongoza India baada ya kuuliwa kigaidi mama yake hapo tarehe 31 Oktoba 1989.
Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa bunge lakini aliuawa na magaidi tarehe 21 Mei 1991 akiwa na umri wa miaka 47 alipokuwa akifanya kampeni za uchaguzi huo huko kusini mwa India. ***
Miaka 26 iliyopita na katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Suharto wa Indonesia alilazimika kujiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 33.
Aliingia madarakani mwaka 1965 baada ya kumpindua Ahmad Sukarno, mwanzilishi wa Indonesia huru ambaye alikuwa amechaguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Uhuru wa kisiasa ulibanwa sana katika kipindi cha utawala wa Suharto. Hata hivyo nchi hiyo ilishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi katika utawala wake katika miongo ya 80 na 90. Pamoja na hayo lakini mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia Mashariki katika mwaka wa 1997 ulianzisha malalamiko na maandamano makubwa ya wanafunzi wa Indonesia na taratibu yakachukua mkondo wa kisiasa uliopelekea Suharto kuondolewa madarakani.
Ufisadi wa kiuchumi uliofanywa na Suharto pamoja na familia yake ulichochea zaidi kuanguka kwa utawala wake, ambako kulitanguliwa na kujiuzulu kwake madarakani. ***