Jumatano, Mei 29, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 20 Mfunguo Pili Dhulqaada 1445 Hijria mwafaka na tarehe 29 Mei 2024.
Miaka 989 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco.
Abu Ali alijifunza mashairi, fasihi na elimu nyingi za kipindi hicho akiwa bado mdogo na baada ya hapo alielekea katika mji wa Qirawan nchini Tunisia kwa shabaha ya kushiriki katika vikao na majlisi za wasomi wakubwa. Kipindi hicho mji wa Qirawan ulikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Andalusia na wasomi wa Kiislamu na wanazuoni wengi mashuhuri walikuwa wakiishi katika mji huo. Mashairi mengi ya malenga huyo yanaakisi vipindi mbalimbali vya maisha yake ya kijamii.
Mshairi huyo aligundua mbinu mpya ya kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 571 iliyopita sawa na tarehe 29 Mei 1453 vikosi vya Sultani Muhammad Fatih, mtawala wa dola ya Othmaniya vilidhibiti bandari ya Constantinople iliyokuwa makao makuu ya Mfalme wa Roma ya Mashariki. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Muhammad. Mwaka 1930 mji wa Constantinople ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, lenye maana ya "mji wa Uislamu" na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki. Mji huo uko magharibi mwa nchi hiyo. **
Katika siku kama hii ya leo miaka 323 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei mwaka 1701 alizaliwa Anders Celsius mwanafizikia na mtafiti wa Sweden. Familia yake ilikuwa ya wasomi na baba na babu yake walikuwa wanahisabati. Celsius alivutiwa sana na elimu ya nujumu na mwaka 1730 alifanikiwa kuwa mwalimu wa somo hilo katika Chuo Kikuu cha Uppsala. Mwaka 1742 alipendekeza kutumika daraja ya kipima joto kwa mujibu wa Celsius, iliyoitwa kwa jina lake. Mpangilio huo ulikubaliwa rasmi na kuanza kutumika duniani mwaka 1945, mwaka mmoja baada ya kufariki dunia mwanafizikia huyo. ***
Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei 1908 helikopta ya kwanza iliruka angani kwa mafanikio. Mtengenezaji wa helikopta hiyo alikuwa Igor Sikorsky, raia wa marekani mwenye asili ya Poland. Utengenezaji wa chombo hicho cha angani ulifungua ukurasa mpya katika mawasiliano na safari za anga. Chombo hicho kilikuwa na sifa kadhaa maalumu zikiwemo za kupaa angani kwa kwenda mbele na kurudi nyuma na pia kuweza kutua na kupaa kikiwa wima. Helikopta hiyo pia iliweza kutulia sehemu moja angani bila kufanya harakati yoyote ile. ***
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita muwafaka na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, ni kilele kirefu zaidi cha silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata. ***