Oct 23, 2024 02:20 UTC
  • Jumatano, tarehe 23 Oktoba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 19 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 23 Oktoba 2024.

Miaka 152 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa.

Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.

Theophile Gautier

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran, alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran.

Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa.

Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.   

Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani.

Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.

Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.   

Vita vya kihistoria vya al-Alamein

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Mirza Jawad Agha Tehrani.

Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea katika miji mitakatifu ya Qum na Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa.

Allamah Mirza Jawad Agha Tehrani alisifika sana kwa uchamungu, zuhudi na kuwapenda sana Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ni Aine Zendegi na Mizanul Matwalib.

Allamah Mirza Jawad Agha Tehrani