Jumatano, Novemba 6, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 04 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 6 Novemba 2024.
Miaka 392 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden.
Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17.
Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648. ***
Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi.
Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika. **
Miaka 164 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alishika madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini Marekani na kupelekea kushindwa waliokuwa wakiunga mkono utumwa.
Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.
Na miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuingia madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Gollam Reza Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi.
Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu tarehe 13 Aban mwaka huo huo akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imepata kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”