Jumanne, 27 Mei, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 29 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria sawa na tarehe 27 Mei 2025.
Katika siku kama ya leo mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi AS mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi.
Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 542 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, Luca della Robbia, msanii mkubwa wa uhunzi wa Italia. Akiwa kijana alijifundisha kazi ya ufuaji dhahabu, hata hivyo aliachana na kazi hiyobaadaye na kujihusisha na uhunzi wa masanamu. Katika kipindi hicho alipata kuunda masanamu na athari mbalimbali za kale. Athari kadhaa za Luca della Robbia zipo katika majengo tofauti ya maonyesho duniani.

Miaka 187 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa.
Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mgunduzi wa vijidudu maradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB.
Daktari Robert Koch alianza kutwalii na kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu.
Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kutwalii magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba.

Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, harakati ya mapambano ya Riffi nchini Morocco dhidi ya mkoloni Muhispania na Ufaransa, ilipata pigo.
Kwa miaka kadhaa Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi, maarufu kwa jina la Amir Muhammad Riffi, kiongozi wa harakati hiyo, alifanya mapambano mengi na wavamizi wa Uhispania huku akifikia ushindi kadhaa. Ushindi wake dhidi ya majeshi vamizi ya Uhispania uliitia khofu Ufaransa. Mwanzoni mwa mwaka 1924 Miladia askari wa Ufaransa waliingia Morocco kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wa Uhispania dhidi ya harakati hiyo ya Riffi.
Katika kipindi hicho askari hao wa Ufaransa walifanya mauaji makubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Aidha baada ya askari vamizi wa Ufaransa na Uhispania kumtia mbaroni Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi walitekeleza jinai kubwa dhidi ya maelfu ya wafuasi Waislamu wa harakati ya Riffi.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita mwafaka na Khordad 6 mwaka 1328 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Allamah Muhammad Qazwini, mwanafasihi, mtafiti na mwanahistoria wa zama hizi wa Iran. Tangu utotoni Allamah Qazwini na kwa msaada wa baba yake, alijifunza masuala mengi kuhusu fasihi na teolojia ya Kiislamu. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi katika uwanja wa fasihi, falsafa na historia.
