Jumamosi, 08 Februari, 2025
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Shaaban 1446 Hijria inayosadifiana na 8 Februari 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 965 iliyopita aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.
Katika siku kama ya leo miaka 869 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Shaaban mwaka 577 aliaga dunia Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika skuli mashuhuri ya Nidhamiya mjini Baghdad na kutokana na kufaulu vizuri masomo yake na maarifa mengi aliyokuwa nayo, alianza kufundisha katika skuli hiyo. Ibn Anbari ameandika vitabu na makala nyingi za kielimu. Kitabu cha al-Asrar al-Arabiyah ni moja ya athari mashuhuri ya alimu huyo.
Katika siku kama hii ya leo miaka 62 iliyopita Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa jeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, yaani tarehe 20 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la vibaraka hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangushwa utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.