Jumapili, 09 Machi 2025
Leo ni Jumapili 8 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1446 Hijria mwafaka na 9 Machi 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 571 iliyopita, sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia, Amerigo Vespucci.
Kwa mara nne Vespucci alifanya safari kuelekea ardhi zisizojulikana ambazo hadi wakati huo zilikuwa hazijawa na majina ambapo kutokana na jina lake (Amerigo), ardhi hizo zikaitwa kwa jina hilo yaani ‘Amerika, au Marekani’.
Ni kwa ajili hiyo ndio maana watu wengi wakamtaja Americo kuwa mvumbuzi asili wa Marekani. Americo Vespucci alifariki dunia mwaka 1512 Miladia.
Tarehe 9 Machi mwaka 1992, yaani miaka 33 iliyopita, Menachem Begin mmoja kati ya waasisi wa utawala haramu wa Israel na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia.
Begin alizaliwa nchini Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake.
Akiwa na umri wa miaka 12, Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baada ya kuhamia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, sawa na mwaka 1942 akateuliwa kuwa kamanda wa taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada kwa jina la "Irgun."
Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyokuwa ikitekeleza mauaji dhidi ya raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao. Alikuwa katili sana dhidi ya raia wa Palestina kiasi kwamba David Ben Gorion ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa utawala haramu wa Israel alisema kuwa Begin ndiye Hitler wa kweli.
Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri.
Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu.
Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.
Katika siku kama ya leo miaka 12 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari ambaye alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu.
Alizaliwa mwaka 1314 Hijria Shamsia katika eneo la Lar nchini Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Mwaka 1332 alielekea Qum kwa ajili ya elimu ya juu ya Kiislamu.
Huko Qum, Ayatullah Musavi Lari aliasisi Kituo cha Kueneza Maarifa ya Kiislamu Duniani ambacho kilikuwa kikisambaza vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha hai za dunia. Mwaka 1372 Hijria Shamsia Academia ya Sayansi ya Jamhuri ya Azarbaijan ilimtunuku shahada ya uzamivu kutokana na taathira kubwa ya vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha ya Kirusi.
Ayatullah Mujtaba Lari aliaga dunia siku kama ya leo tarehe 19 Esfand katika Hospitali ya Imam Ridha (as) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa kipindi kirefu.